ELIMU
   
Rudi nyumbani
................................................................................................................................. ................................................................................................................................. .................................................................................................................................
         
 
UTANGULIZI
 
 
Bw. T. MASSAWE
Afisa Elimu - Mkoa wa Kilimanjaro
 
Mkoa una jumla ya shule za Awali 746, kati yake 683 ni za serikali na 63 zisizo za serikali. Shule za Msingi zipo 915, kati ya hizo shule za serikali ni 880 na shule zisizo za serikali ni 35. Kwa mwaka 2008, mkoa ulikuwa na jumla ya shule za sekondari 295, ambapo shule 206 ni shule za serikali na shule 89 ni shule zisizo za serikali. Pia, mkoa unazo taasisi nyingine za kutolea elimu kama ilivyoainishwa katika jedwali A. BONYEZA HAPA
 
1.1 MPANGO WA MAENDELEO YA ELIMU YA MSINGI
 
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) umewezesha kuongezeka na kuimarishwa kwa miundombinu ya kutolea elimu na kufanya watoto wote wenye umri wa kwenda shule kupata nafasi katika shule zilizopo mkoani. Kutokana na MMEM kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule za msingi. Uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka 2008 ulifikia 44,461 sawa na asilimia 106 ya lengo. Idadi ya shule za msingi ziliongezeka kutoka 896 mwaka 2006 hadi 915 mwaka 2008. Kati yake 880 ni za serikali na 35 zisizo za serikali.
 
Mkoa una jumla ya wanafunzi 335,180 wa darasa la I – VII, wakiwemo wavulana 169,983 na wasichana 165,197. ‘Gross Enrolment Rate' (GER) ni asilimia 105.4 na ‘Net Enrolment Rate' (NER) ni asilimia 96.
 
1.2 Elimu ya watoto wenye ulemavu
 
Katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), kila Halmashauri imekuwa ikitoa huduma kwa wanafunzi wenye ulemavu kulingana na ulemavu uliopo. Vipo vituo/shule 21 vyenye watoto 701 wenye ulemavu mbalimbali.
 
Hali ya upatikanaji wa huduma za Elimu ya Msingi ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali lifuatalo: BONYEZA HAPA
 
1.3 Vyumba vya madarasa
 
Mahitaji ya vyumba vya madarasa katika mkoa ni 8,117. Vyumba vilivyopo ni 6,688 sawa na asilimia 82.4. Kila wilaya imeelekezwa kutumia rasilimali walizo nazo kupambana na upungufu huu wa madarasa.
 
1.4 Nyumba za walimu
 
Mahitaji ya nyumba za walimu wa shule za msingi ni 10484 na idadi ya nyumba zilizopo ni 1,110 sawa na asilimia 10.6 tu ya mahitaji ya mkoa.
 
Pamoja na jitihada za serikali katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi kujaribu kupunguza tatizo hilo , bado tuna changamoto ya kushirikisha wadau mbalimbali katika mkoa ili kujenga nyumba zaidi za walimu, na majengo mengine.
 
1.5 Madawati
 
Mkoa unahitaji madawati 157,024 na madawati yaliyopo ni 134,623 sawa na asilimia 85.7 ya mahitaji.
 
 
Juhudi zaidi zinahitajika kutoka kwa wadau wote ili kuondoa upungufu wa madawati 22,401 uliopo pamoja na samani nyingine.
 
1.6 Walimu
 
Idadi ya mahitaji ya walimu wa shule za msingi katika mkoa ni 10484, waliopo ni 8735 sawa na asilimia 83.3.
 
Kwa kawaida tathmini ya Taaluma katika Elimu ya Msingi inafanyika kwa kutumia mtihani wa darasa la VII. Kwa kutumia kigezo hicho, hali ya taaluma kwa miaka mitatu iliyopita ni kama ifuatavyo: BONYEZA HAPA
 
Baada ya kuona kuwa kiwango cha ufaulu mwaka 2007 katika mkoa kimeshuka, Mkoa uliitisha kikao cha wadau wa elimu kwa ajili ya kujadili na kuweka mikakati ya kuinua kiwango cha kufaulu.
 
2.0 MPANGO WA MAENDELEO YA ELIMU YA SEKONDARI
 
2.1 ELIMU YA SEKONDARI
 
Wananchi kwa kushirikiana na serikali na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali wameweza kujenga shule nyingi, kwa mfano mwaka 2007 shule mpya za sekondari za kutwa 71 zilijengwa na kufunguliwa.
 
Mkoa una jumla ya shule za kutwa 207 zilizopokea wanafunzi wa kidato cha I – 2009. Shule hizi zina jumla ya mikondo 1100 iliyo tayari na mingine 414 inayoendelea kujengwa. Idadi ya shule za bweni ni 9. Zipo shule 89 zisizo za serikali.
 
2.2 MTIHANI WA KIDATO CHA IV – 2008
 
Idadi ya watahiniwa wa shule imeongezeka kutoka 13,918 mwaka 2007 hadi 16,255 mwaka 2008, ongezeko la watahiniwa 2,337 sawa na asilimia 14.
 
2.3 MAPENDEKEZO YA KUANZISHA MADARASA YA KIDATO CHA TANO NA SITA
 
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kufaulu kuingia kidato cha tano, mkoa unajizatiti kujenga angalao shule moja ya kidato cha 5 na 6 (A Level) katika kila tarafa. Shule zenye ‘A Level' zipo 52 kati yake 14 ni za serikali na 38 zisizo za serikali. Jumla ya shule 34 katika wilaya zote zimeteuliwa kuandaliwa kuanzisha vidato hivyo.
 
2.4 WALIMU SHULE ZA SEKONDARI ZA SERIKALI
 
Mkoa unao upungufu mkubwa wa walimu wa sekondari wapatao 608,
 
3.0 VYUO VYA UALIMU NA MAENDELEO YA WANACHI :
 
Mkoa una jumla ya vyuo vya ualimu 7, kati yake vyuo 3 ni vya serikali na vyuo 4 visivyo vya serikali.Vyuo hivi vinatoa mafunzo ya cheti na stashahada ya ualimu.
 
 
 
Pia vipo vyuo vya maendeleo ya wananchi 3. Mtawanyiko wa vyuo hivi ni kama ilivyo kwenye jedwali A.
 
4.0 VYUO VYA VETA:
 
Mkoa unacho chuo cha kanda cha VETA pamoja na vyuo vingine 70 vilivyo kwenye wilaya zetu. Vyuo hivi vinatoa mafunzo kwenye nyanja mbalimbali za utoaji huduma za ujasiriamali, hoteli na utalii, sekta za uzalishaji (manufacturing) na sekta ya ujenzi (construction).
 
5.0 VYUO VIKUU:
 
Mkoa una vyuo vikuu 5, kati yake vyuo vikuu 2 ni vya serikali na 3 visivyo vya serikali.
 
6.0 CHANGAMOTO ZINAZOUKABILI MKOA KATIKA UTOAJI WA ELIMU BORA
 
6.6.1 Mkoa una mahitaji makubwa ya vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari ili kupunguza msongamano katika chumba cha darasa. Pia upo uhaba mkubwa wa nyumba za walimu, ambapo nguvu za pamoja kati ya jamii na serikali zinatakiwa ilikumaliza matatizo yaliyopo.
 
Mpango wa kuanzisha vidato vya 5 na 6 umeshaanza japo kasi ya kukamilisha madarasa na hosteli siyo kubwa kama ilivyotarajiwa. Hii ni kutokana na wananchi kutopenda kuchangia ujenzi kwa vile shule inapokamilika inapokea wanafunzi toka pande mbalimbali za nchi bila ubaguzi. Wanasahau kuwa hata watoto wao wanasoma katika shule ambazo hawakuzichangia. Bado tuna kazi ya kuwaelimisha ili wakubali kuchangia kwa moyo.
 
Walimu wanaopangwa kufundisha katika shule zilizo mbali na mji au na barabara kuu hukataa kwenda kufundisha shule hizo kutokana na kuwa na miundombinu hafifu, hii ni pamoja na ukosefu wa nyumba za walimu, mawasiliano duni, ukosefu wa maji na umeme.
 
Bado mkoa una tatizo kubwa la miundombinu ya kutolea elimu. Iliyopo haitoshelezi na pia mingine imeshaanza kuchakaa na kuhitaji ukarabati.
 
Tuna tatizo kubwa la walimu hasa wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule za sekondari. Pia upo uhaba mkubwa wa maabara na maktaba, hivyo kufanya masomo ya sayansi kufundishwa kwa nadharia tu.
 
Upo pia uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwenye shule za msingi na sekondari. Tunahimiza walimu kuandaa zana za kufundishia kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao na walimu wabunifu huzawadiwa.
 
Kwa ujumla kila kata katika mkoa huu ina shule ya sekondari ya serikali. Kwa kuwa kata nyingine zimepanuka sana na kwa kuzingatia Geografia ya mkoa huu ya milimamilima, tunahimiza wananchi kujenga hosteli ili wanafunzi wanaotoka mbali waweze kupata mahali pa kuishi na kupata muda mwingi zaidi wa kujisomea
         
Rudi juu   Rudi juu   Rudi juu
 
.........................................................................................................................................................................................................................................................................................
 
COPYRIGHT© OFISI YA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO, S.L.P 3070, SIMU: 027 2752184/54236-7, FAX: 027-2753248. HAKI ZOTE ZIMEHIFADHIWA.