NIMEDHAMIRIA KUMSAIDIA RAIS KATIKA KILIMO - WAZIRI MKUU
           
       
   
     
     
......................................................................................................................................................................................................................................................................................
     
     
     
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema amedhamiria kumsaidia Rais Jakaya Kikwete katika kampeni yake ya kuinua kilimo ili kiweze kubadili maisha ya Watanzania.
 
Akizungumza na wakazi wa Mabogini mara baada ya kutembelea skimu wa umwagiliaji ya Lower Moshi na kituo cha mafunzo ya kilimo cha Kilimanjaro (KATC), Waziri Mkuu alisema mradi huo ni mkubwa mno ambao unahitaji uwekezaji wa Serikali ili uweze kufanikiwa kuleta mabadiliko ya kilimo kwa wakazi wa eneo hilo.
 
 
PICHANI : Mojawapo ya miundombinu ya umwagiliaji katika mradi wa umwagiliaji - Lower Moshi
 
Alitoa kauli hiyo baada ya kukagua mradi wa umwagiliaji mashamba ya mpunga ulioko kata za Mabogini na Kahe wilayani Moshi Vijijini. Mradi huo ambao unahusisha vijiji vinne vya Mabogini, Rau Kati, Chekereni na Oria una hekta 2,300 lakini zinazotumika kwa sasa ni hekta 1,100 kwa vile zimejengewa miundombinu ya umwagiliaji mpunga na hekta 1,200 zilizobaki zinatumika kwa mazao mengine.
 
“Huu mradi ni mkubwa mno na juhudi ambazo zimefanywa na Serikali hadi sasa ni kidogo mno… hii ni changamoto kwa Serikali lakini lazima tukubali ukweli kuwa kama mifereji haikutengamaa, hakuna maji ya kutosha mtakayopata ili kuendeleza kilimo katika eneo lote hili ,” alisema
 
Alisema taarifa aliyopokea inaonyesha uchakavu wa mitambo na pampu za maji katika mradi huo unachangia upotevu mkubwa wa maji kwa hiyo mradi mzima inabidi uangaliwe upya kuanzia ngazi za mkoa na hadi Serikali Kuu.
 
“Huu mradi ni sawa na mgonjwa aliye katika katika comma (mahututi) hatujui kama atapona au atakufa… Serikali inatakiwa ijipange vizuri, iweke mambo sawa ndipo iweze kupata ufumbuzi wa jinsi ya kuendesha mradi kwa faida ya wananchi,” alisema.
 
Akifafanua zaidi alisema: “Ili kuuokoa mradi huu, inabidi nikirudi tukae na wataalamu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji watuambie katika bajeti ijayo wamepanga kufanya nini na mradi huu kwa sababu tulizembea,…kwa miaka 20 hakuna msukumo uliowekwa kuundesha mradi huu…”.
 
Alisema faraja pekee aliyonayo ni watu aliowakuta mashambani wakifanya kazi kwa kujituma na baadhi ya mashamba aliyoyaona yamepandwa kwa kufuata mistari. “Hii ni dalili njema kuwa watu wanafanya kazi vizuri… mwamko wenu ndiyo faraja pekee… naondoka hapa nimepata hamu ya kuimarisha mradi huu,” alisema huku akishangiliwa.
 
Alisema ili kufanikisha azma hiyo, inabidi viongozi wajinyime ili hizo fedha zilizotengwa kwa ajili yao ziwasaidie wakulima. “Uamuzi wa kuzuia magari na semina ni mtihani mkubwa kwa Serikali lakini inabidi tubadilike kwa sababu kwa staili hii hatuwezi kusukuma nchi ikaenda mbele… ifike mahali tuseme hapana!,” alisisitiza.
 
Alisema ununuzi wa magari ambao ataruhusu ufanyike ni yale ya kusaidia miradi ya kilimo kama huo ili wataalamu wawafikie wananchi kwa urahisi. “Iweje kila siku tuwaambie wananchi kazaneni katika kilimo lakini wewe kama kiongozi hauko tayari kukazana kujinyima starehe?” alihoji.
 
Waziri Mkuu ambaye pia alijibu kero mbalimbali za wananchi aliwahimiza kupitia ushirika wao wachague viongozi makini watakaosimamia mradi kwa faida ya wananchi na si wao binafsi. “Tukiwa na usimamizi makini na viongozi makini tutahakikisha kila mwenye boda (jaluba) anaitumia ardhi kwa mujibu wa makubaliano.”
 
Kuhusu ukosefu wa soko la mchele wanaozalisha, alisema tatizo la soko la uhakika litakwisha kama wataamua kuanzisha mpango wa stakabadhi ya mazao ghalani ambao lazima ukubalike na wote kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa.
 
Pia aliwahimiza kujikinga na maambukizi ya virusi ya virusi vya UKIMWI na magonjwa ya zinaa kwa sababu eneo wanaloishi ni miongoni mwa maeneo yenye msukumo wa maendeleo kwa sababu ya uzalishaji mkubwa wa mpunga unaofanyika hapo na biashara ya mchele inayoendelea.
 
rudi nyuma
     
© 2008 OFISI YA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO, S.L.P 3070, SIMU: 027 2752184/54236-7, FAX: 027-2753248   Rudi juu