MAELEZO KUHUSU HALMASHAURI YA WILAYA YA ROMBO

 UTANGULIZI

Wilaya ya Rombo ilianzishwa tarehe 1 Julai 1972 kwa kuimega Wilaya ya Moshi. Wilaya hii ni moja kati ya wilaya sita (6) zinazounda mkoa wa Kilimanjaro. Wilaya nyingine ni Hai, Siha, Same, Mwanga, Moshi Vijijini , aidha mkoa una manispaa moja.

UTAWALA

Wilaya ina tarafa 5, kata 20, vijiji 60 na vitongoji 295.  Baraza la Madiwani linaundwa na madiwani 30 ikiwa ni pamoja na Mbunge wa Jimbo na Mbunge Viti Maalum.  Madiwani 28 ni wa CCM na 2 ni wa CHADEMA.

ENEO NA MIPAKA

Eneo

Ukubwa wa Wilaya ni Kilometa za mraba 1,442 au Hekta 144,200.  Eneo kubwa  la  mlima Kilimanjaro na vilele vyake viwili (Kibo na Mawenzi) liko ndani ya Wilaya ya Rombo.

Hk 44,144 zinafaa kwa kilimo; Hk 57 zinafaa kwa ufugaji;  Hk 38,194 ni misitu ya asili na ya kupandwa na Hk 16,692 ni za  malisho ya mifugo. Hk 45,113 ni eneo la maji,milima na  miamba. 

Mipaka

Wilaya inapakana na nchi ya Kenya kwa upande wa Kaskazini, upande wa Mashariki inapakana na Wilaya ya Moshi, upande wa Magharibi inapakana na Wilaya ya Hai na Kaskazini Magharibi ipo Wilaya ya Loliondo.

IDADI YA WATU NA MGAWANYO WA KIUTAWALA

Idadi ya Watu

Idadi ya watu kwa mwaka 2008, ilikadiriwa kuwa jumla ya watu 267,092 kwa kukokotoa matokeo ya sensa ya kitaifa ya mwaka 2002 ya watu 245,749 na ongezeko la 1.4% kwa mwaka.  Msongamano wa watu kwa kilometa moja ya mraba; ni kati ya watu 200 Ukanda wa Chini na watu 500 Ukanda wa Juu.  Hali hii imesababisha uhaba mkubwa wa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji, ujenzi wa huduma za jamii kama shule, zahanati, vituo vya afya, masoko, viwanja vya michezo na shughuli za uwekezaji viwanda, hoteli, n.k.

Aidha Wilaya ya Rombo ina jumla ya watumishi wapatao 2,529. Halmashauri ya wilaya watumishi 2,220 na wa Serikali Kuu 309.

 

MWELEKEO WA HALMASHAURI (DHIMA)

Halmashauri itajiendesha kwa misingi ya utawala bora ikiwashirikisha wadau wote katika kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na ya kijamii kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa njia endelevu na kwa kuzingatia vipaumbele vinavyopangwa na jamii.

Dira ya Halmashauri

Kuwa wilaya inayotoa huduma bora na yenye jamii inayojitosheleza kwa mahitaji ya kiuchumi na kijamii na inayoishi kwa amani na utulivu.

UCHUMI WA HALMASHAURI

Uchumi wa wilaya unategemea kilimo, ufugaji, mazao ya misitu na madini ya pozollana.

VYANZO VIKUU VYA MAPATO YA HALMASHAURI

Uendeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo unategemea sana vyanzo vyake vya Ndani vya Mapato. Vyanzo vikuu  ni ushuru wa kahawa, ushuru wa Pozzolana na ushuru wa magogo. Hali halisi ya mapato katika mwaka wa fedha 2004/05 ilikuwa ni Tshs 218,572,354.00 kati ya lengo la Tshs 306,038,400.00 sawa na 71%. Mwaka 2005/06 makusanyo yalikuwa Tshs 146, 609,924.00 kati ya lengo la Tshs 310,178,000.00 sawa na 47%. Sababu za kushindwa kufikia lengo ni uzalishaji mdogo wa zao la kahawa na Kampuni ya Tanga Cement kuchukua Pozzolana kidogo kuliko tulivyokadiria.

Mapato ya vyanzo vya ndani yameongezeka kutoka Tshs. 140,000,000/= mwaka 2004 hadi shs. 400,000,000/= mwaka 2008.

Ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kwa mwaka 2007/2008 ulikuwa mzuri. Lengo lilikuwa kukusanya shs. 554,340,416.67. Mpaka mwezi Juni 2008 zilikusanywa shs. 624,371,621.13 sawa na asilimia 103.25 ya lengo la mwaka.

Mapato ya Serikali Kuu

Makusanyo ya kodi za ndani 2007/2008 yalikuwa Tshs.456,930,659.00 sawa na asilimia 175. Lengo lilikuwa kukusanya Tshs 261,519,560.00

Makusanyo ya ushuru wa forodha vituo vya Holili na Tarakea yalikuwa shs.22,106,863,865.70 sawa na asilimia 81.8 ya lengo la kukusanya shs.27,005,000,000.00.

Ufungaji wa hesabu za Halmashauri umekuwa ukifanyika ndani ya muda uliowekwa kisheria.  Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali za halmashauri yetu ni nzuri.

KILIMO NA MIFUGO

Hali ya hewa

Wilaya haipati mvua za kutosha hivyo hukumbwa na ukame wa mara kwa mara.

Wilaya inazo jumla ya Hk. 281 za umwagiliaji wa mazao mbalimbali kama kahawa/migomba, mboga, mahindi, maharage, kunde, karanga na ulezi.

Shughuli kubwa zinazofanywa na wananchi wa wilaya ya Rombo za kujipatia kipato ni kilimo, ufugaji, na biashara. 

Mipango iliyopo inalenga katika kuongeza wingi na ubora wa mazao ya mimea na mifugo.

Kahawa

Zao kuu la biashara ni kahawa inayolimwa na wakulima kwenye vishamba vidogo.  Tunao wakulima wadogo 30,000 wenye jumla ya hekta 10,000.  Lengo ni kila hekta izalishe kilo 600 ifikapo mwaka 2010; na gharama za uzalishaji ziwe wastani wa shs. 410,000/- kwa hekta.  Mkakati wa kufikia malengo haya ni kuotesha kahawa chotara (clonal coffee) miche 7,500,000 ifikapo mwaka 2010.  Tunazo bustani mama 21 zenye miche 7,500 ya kahawa chotara.  Bustani hizi zitazalisha miche 525,000 ya kahawa kwa mwaka. 

Wilaya inazo jumla ya Hk. 15,837 za kahawa ambazo zimepandwa pamoja na migomba. Kwenye mashamba ipo mibuni ya kahawa 11,315,689, kati ya hiyo asilimia 20 imezeeka  sawa na mibuni  2,263,138.

Vimemeanzishwa vikundi  vya wakulima na tunashirikiana kwa karibu na taasisi za dini kuboresha kilimo cha kahawa.

Shughuli ya kuiondoa na kuiendeleza  mibuni ni kama ifuatavyo:-

Kung’oa asilimia 10  kwenye Hk 170.

Stumping asilimia 25 kwenye Hk 383.

Kuendelea kuotesha asilimia 25 kwenye Hk 791.85.

Kuendeleza miche michanga asilimia 10 kwenye Hk 1,583.7.

Chakula

Lengo la kila mwaka ni kuzalisha mazao ya chakula ya kutosha na ziada kwa biashara.  Mazao haya ni ndizi, mahindi, maharage, viazi, mhogo, ulezi, mbaazi na alizeti.  Mahitaji yetu ya chakula kwa mwaka ni tani 38,576 za wanga na tani 19,288 za protini.

Matarajio ya wilaya ni kupanua kilimo cha matunda, uyoga na ufugaji wa nyuki ili kuwaongezea wakulima wetu kipato.  Uzalishaji wa kutosha unahitajika ili kuweza kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao.

Mwaka 2007/2008 zilivunwa wanga tani 196,685 na protini tani 3,921.  Chakula kingi kilizalishwa ukanda wa juu; ambao wakazi wake wengi walijitosheleza na waliuza ziada.

Wakulima wa Ukanda wa Chini wanashauriwa kuzingatia zaidi kilimo cha mhogo na mbaazi.

Ili kuongeza usalama wa chakula, wananchi wanahimizwa kuotesha mihogo, magimbi, viazi vitamu, viazi vikuu.  Aidha wametakiwa kuwa na hifadhi ya chakula.

Ushirikiano na taasisi za Tengeru na SUA umewezesha kupanua kilimo cha maparachichi aina ya Alfonso. Miche 9,000 imeshaoteshwa na yapo matarajio ya kuongeza miche 3,000 msimu ujao. Msimu huo pia kuna matarajio ya kuotesha miche 4,000 ya maembe.

Ndizi

Lengo ni kuongeza uzalishaji hadi tani 236,850 kwa mwaka ili kuongeza pato la wakulima.  Aina ya ndizi tunazozipa kipaumbele zinazalishwa kwa teknolojia ya “tissue culture”.  Mwaka 2007/2008 hekta 24 zilistawishwa na zilizalisha tani 351 za ndizi. 

Vipindi virefu vya unyaufu na fursa ndogo za kuendesha kilimo cha umwagiliaji zinadumaza mafanikio ya kilimo hiki.   Utaratibu mzuri wa kuwa na soko la uhakika la ndizi ili wakulima  wapate bei nzuri unahitajika.

 

 

Matunda

Lengo ni kupanua kilimo cha maparachichi aina ya “hass” na maembe aina ya “alfonso” kwa ajili ya lishe na biashara.  Kuotesha miche 20,000 ya maparachichi na 25,000 ya maembe yatakayozalisha tani 4,320 za matunda haya na kuwaingizia wakulima shs.216,000,000.00 kwa mwaka ifikapo mwaka 2010.

Mifugo

 

Lengo la Wilaya ni kuwa na mifugo bora inayotoa nyama, maziwa na mayai kwa wingi.  Uzalishaji wa nyama  uongezeke kwa mwaka kutoka kilo 1,350,461 za sasa hadi kilo 1,620,553; maziwa yaongezeke kwa mwaka kutoka lita 15,769,976 hadi lita 21,350,121. Mayai yaongezeke kwa mwaka kutoka 21,090,631 hadi 42,181,262;  ifikapo mwaka 2010.

Wilaya ina ng’ombe wa kisasa 22,636 na ng’ombe wa kienyeji 37,200. Mbuzi wa kisasa na kienyeji 135,248.  Tatizo kubwa linalowakabili wafugaji ni kupata malisho kwani mifugo hufugwa ndani na ukame wa  mara kwa mara  unaoathiri malisho ukichangiwa na uhaba mkubwa wa ardhi.

Zaidi ya asilimia 90 ya Wakazi wa Wilaya hii ni wafugaji wadogo. Wanyama wanaofugwa ni kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku na sungura.

Asilimia kubwa ya ng’ombe na mbuzi wa maziwa hufugwa katika Ukanda wa Juu na Ukanda wa Kati. Hali ya hewa ni nzuri na mchanganyiko wa malisho hupatikana kwa wingi.  Mifugo hii hufugwa ndani na uzalishaji wa maziwa ni wastani wa lita 5 kwa siku. Ng’ombe wa kienyeji hufugwa kwa wingi Ukanda wa Chini na hutoa wastani wa lita 2 za maziwa kwa siku.

MALIASILI NA MAZINGIRA

Misitu

Tuna misitu ya aina 3. Msitu wa Lindimaji (Water-Catchment Forest). Msitu wa Nusu Maili na Msitu wa Rongai. Msitu wa Lindimaji unahifadhiwa na KINAPA. Wananchi wa vijiji jirani wanashiriki katika ulinzi wa msitu na hufaidika na misaada ya ujirani mwema toka KINAPA. Msitu wa Nusu Maili una Hk. 3,200 na unasimamiwa na Halmashauri. Programu ya kuotesha miti katika eneo lote itakamilika mwaka 2009. Shamba la Miti Rongai lina ukubwa wa Hk. 6,200 na uwezo wa kuuza mita 25,000 za ujazo za magogo kwa mwaka bila kuathiri uendelevu.

Lengo ni kuotesha miti laini kwa ajili ya mbao na kuzipatia Halmashauri na Serikali Kuu mapato.  Eneo lote la Halmashauri litamalizika kuoteshwa miti mwishoni mwa mwaka 2009.  

Wilaya ina vikundi 22 vya ufugaji nyuki. Huzalisha asali na nta. Huzalisha kiasi cha kg. 2,000 za asali kwa mwaka ila lengo ni kufikia hadi kg. 12,000 ifikapo mwaka 2010.

Jumla ya mizinga ni 3,981 na inamilikiwa na vikundi vya kina mama/vijana na watu binafsi.

Hifadhi ya Mazingira

Hifadhi  ya mazingira imegawanyika sehemu tano.  Ambazo ni  Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro;  Msitu wa Lindimaji (water catchment forest); Msitu wa Nusu Maili; Mashamba ya Wananchi na machimbo ya pozollana.

Lengo la wilaya ni kudhibiti moto kwenye Hifadhi ya Mlima, kuhifadhi Msitu wa Lindimaji, kuotesha miti eneo lote la Nusu Maili na mashamba ya wananchi.  Kwenye machimbo ya  pozollana  Kampuni ya Saruji Tanga ina utaratibu wa kuchimba na kufanya ukarabati wa eneo baada ya kuchimba.

Vijiji 14 vimeingia mkataba wa usimamizi shirikishi katika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira.  Maeneo yanayochimbwa mawe, mchanga na morrum yanakarabatiwa kwa kurudishia udongo na kuotesha miti. Aidha   wananchi wanaoshi karibu na msitu wanashiriki kuzima moto mara unapotokea ndani ya msitu.

Kazi ya kuimarisha Kamati za Mazingira za vijiji inaendelea ili zisimamie  sheria ndogo za mazingira, na kudhibiti shughuli za binadamu kwenye maeneo yote ya hifadhi.

Elimu ya hifadhi ya mazingira inaendelea kutolewa kwa wananchi katika mikutano ya hadhara kwa kushirikiana na Taasisi zisizo za Kiserikali kama TECOSO na KEDA. 

Doria 120 zimefanywa katika misitu na mpakani na nchi jirani ili kuzuia wanyama waharibifu.

 

 

 

USHIRIKA, VIWANDA NA BIASHARA

Wilaya ina Vyama vya Ushirika vya Msingi 16; vya  Akiba na Mikopo 16 na Ushirika wa Viwanda 1. Vina jumla ya wanachama 34,290.

Mikopo yenye thamani ya Tshs. 14.0m ilitolewa kwa SACCOS  7 na SACAS 2.

Wajasiriamali 173 walipata mikopo yenye thamani ya Tshs. 210,025,000/= kutoka fedha za uwezeshaji wananchi NMB na CRDB.

Lengo ni kuhamasisha wanachama wapya na kuongeza akiba, na amana ya vyama hivi.  Aidha kuimarisha ukaguzi na elimu kwa wanachama.

Biashara na Masoko

Kuwa na soko la nafaka maeneo ya mpakani Holili na Tarakea; ifikapo mwaka 2010.  Aidha kuvijengea uwezo vikundi 407 na kuviunganisha na masoko; na kuwa  na vituo 5 vya upatikanaji wa taarifa za masoko.

Tumefanikiwa kujenga soko moja Tarakea na kuvijengea uwezo vikundi 42.

Ukosefu wa maeneo ya kuanzisha masoko na fedha za kuyajenga vinaviza  juhudi hizi.

Utalii

Wilaya ina njia moja ya watalii ya kupanda mlima Kilimanjaro huko Nalemuru. Shughuli za utalii zinatarajiwa kuongezeka ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami utakapokamilika.

Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mamtukuna kinaendeleza utalii wa utamaduni na mazingira (eco-cultural tourism) na nchi ya Sweden. Kivutio kipya cha utalii kinatarajiwa kuwa ni Ziwa Challa (crater lake). Hapa panatarajiwa kuwepo na bustani ya ufugaji wa wanyamapori.

Viwanda Vidogo

Wilaya ina viwanda vidogo 40 vya kupasua mbao na 3 vya kusindika mafuta. Msukumo mpya umewekwa kwa kushirikiana na SIDO katika kuendeleza viwanda hivi wilayani. Viwanda hivi vinatarajiwa kusindika mazao ya kilimo na kuendeleza mafunzo kwa vitendo. Fursa zilizopo za kuliwezesha jambo hili ni pamoja na kuweko kwa umoja wa mafundi wilayani (Rombo DALTA) na mazao ya kilimo yanayozalishwa.

 

 

BARABARA

Wilaya in mtandao wa km. 593 za barabara. Kila kitongoji kinafikiwa kwa gari. Barabara Kuu ina urefu wa  km. 75. Barabara za Mkoa km.56. Barabara za wilaya km. 257 na za vijiji km. 205. Barabara kuu ya Marangu/Kilacha – Kamwanga inajengwa kwa kiwango cha lami. Wananchi wa vijiji vyote wamejiwekea utaratibu wa kutunza barabara za vijiji na vitongoji na changamoto kubwa ni jinsi ya  kudhibiti maji ya mvua yanayosababisha uharibifu wa haraka wa barabara hizo.

Ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami umekamilika sehemu ya kwanza km. 32.  Sehemu ya pili km. 33 inaendelea kujengwa na sehemu ya tatu km. 32, iko kwenye maandalizi. 

Simu

Huduma za simu zimesambazwa sehemu zote Wilayani. Hizi ni pamoja na simu za mikononi.  Pamoja na huduma za Shirika la Posta na Simu makampuni mengine ni yale ya  Simu za Mikononi likiwemo VODACOM, TIGO na ZAIN.  Ndani ya wilaya pia kuna Radio Calls.3.

MAJI

Mtandao wa bomba za maji wilayani una jumla ya urefu wa Km.1,050. 

Wilaya ya Rombo ina vyanzo vya maji 30 vinavyotoa wastani wa mita za ujazo 20,000 kwa siku.  Kiwango cha huduma kinakadiriwa kufikia kati ya 65% - 70% kwa nyakati za kawaida.  Maji hayo hupungua nyakati za kiangazi hadi kufikia mita za ujazo 15,000 kwa siku.  Kuanzia mwaka 2001 wafadhili wa GTZ wamesaidia mpango wa kuondoa mabomba ya zamani yenye kipenyo kidogo na kuweka mabomba mapya yenye kipenyo kikubwa kuanzia chanzo cha maji huko Marangu.  Asilimia 70 ya wakazi wa Rombo ndio wanapata maji safi na salama. Upatikanaji wa maji kwa sasa ni wastani wa lita  12,335,000 kwa siku ukilinganisha na mahitaji halisi ambayo ni lita 28,000,000 kwa siku.

Katika mwaka 2007/2008 miradi ya maji yenye thamani ya shs.244,806,000.00 ilijengwa na kukamilika.

Wilaya inao Mradi wa ukarabati utakaogharimu Euro 6.4m (Tshs.10.24).  Mradi huu ulitegemewa kumalizika mwishoni mwa mwaka 2008 na ungeongeza meta za ujazo 5,700 kwa siku katika mtandao wa sasa.

Lengo la Wilaya ni kuongeza asilimia ya watu wanaopata maji safi na salama kutoka 70% hadi 90%.

Tunaendeleza teknolojia ya kuvuna maji ya mvua na mwaka 2008/2009 yatajengwa matanki 20 yenye ujazo wa jumla ya lita 100,000 Ukanda wa Chini. Changamoto ni kupata vyanzo vya kuongeza maji kwenye mtandao wa mabomba tulionao.  Changamoto nyingine ni kutumia maji kutoka Ziwa Challa.

Kamati  53 za maji kati ya kamati 73 zimepewa mafunzo.

ELIMU

Elimu ya Awali

Lengo ni kuwa na madarasa ya awali katika shule zote za msingi 156.

Wilaya ina madarasa ya awali 159.  142 ni ya serikali. 17 ni ya binafsi.

Elimu ya Msingi

Wilaya ina shule 156 za msingi (moja ni ya taasisi). Zina jumla ya wanafunzi 67,828. Wilaya ina mahitaji ya walimu 1,893.  waliopo ni 1,501.  Upungufu ni walimu 392 sawa na asilimia 21. Upungufu mwingine ni madarasa 441, nyumba za walimu 1,650, vyoo (matundu) 11,121, madawati 4,790, meza 740 na kabati 546.

Darasa la IV walifanya mtihani wanafunzi  7,761; wakafaulu 7,465 (96%). Walichaguliwa  7,465 (96%).

Darasa la VII walifanya mtihani 11,887; wakafaulu 7,645 (64%). Walichaguliwa  7,645 (100%).

Watoto 8,322 waliandikishwa darasa la kwanza mwaka 2008 kati ya waliotazamiwa 7,625.  Hii ni sawa na 109.14%

Msongamano darasani umepungua,  kiwango cha utoro kimepungua na kiwango cha kufaulu kimepanda kutoka asilimia 42 hadi 65. Aidha shule zote hutoa chakula cha mchana.

 

Elimu ya Sekondari

Wilaya ina shule za sekondari 47. 40 ni za serikali na 7 ni za taasisi. Shule 22 ni shule mpya zenye mikondo minne minne. Kwenye kata nyingine ujenzi umekuwa mgumu kutokana na uhaba wa ardhi hivyo kulazimika kujenga majengo ya  ghorofa.

Kati ya shule 47; 34 hazijawa na kidato  hadi cha nne.  Lengo ni kuendelea na ujenzi wa madarasa, maabara na nyumba za walimu kwa shule zote mpya.

Vyumba 70 vya madarasa ya sekondari vimejengwa. Vyumba 8 katika shule za “A” level”.

Shule 5 za kutoa mafunzo ya kidato cha V na VI zimebainishwa nazo ni: Horombo, Kisale, Makalema, Matolo na  Mahida.

Hosteli moja inajengwa sekondari ya Mahida

Elimu ya Watu Wazima

Chini ya Mpango wa MEMKWA kuna wanafunzi 264 katika vituo 17. Wanafunzi 48 walifaulu kuingia darasa la V mwaka jana. Mwaka huu watakaofanya mtihani wa darasa la IV ni 181 na la VII ni 83. Vipo vituo 21 vya MUKEJA vyenye wanafunzi 2,969. Matarajio ni kuwa mwakani tutakuwa na jumla ya vituo 30.

AFYA

Wilaya ina hospitali 2, vituo vya afya 5 na zahanati 34.  Hospitali zote 2 zinamilikiwa na Kanisa Katoliki.  Kulingana na mpango wa Serikali wa kuwa na zahanati kwenye kila kijiji na kituo cha afya kwenye kila Kata, tumeanza kutekeleza mpango huo kwa kuanza ujenzi wa zahanati 6 na vituo vya afya 2.  Upungufu uliopo ni wa zahanati 16 na vituo  vya afya 15.

Malengo ya Wilaya ya huduma za afya ni kuimarisha kinga na tiba dhidi ya malaria; kupunguza vifo vya uzazi na watoto walio chini ya miaka 5, kutokomeza ugonjwa wa vikope, kumaliza tatizo la utapiamlo, kuimarisha afya ya jamii ya msingi na kuongeza wanachama wa Bima ya Afya.

Vifo vya watoto wachanga waliozaliwa hai vimepungua kutoka 39/1000 hadi 10/1000.  Vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kutoka 21/1000 hadi 5/1000.  Vifo vya uzazi vimepungua kutoka 104/100,000 hadi 84,100,000.  Wazazi wanaozalishwa na wakunga waliopata mafunzo wameongezeka kutoka asilimia 67 hadi 70. Kiwango cha ubora wa vyoo kimepanda toka 65% hadi 72%. Kiwango cha chanjo kimefikia 90%.

Maambukizi ya malaria yalipungua hadi 20% . Vyandarua  9,000 vyenye viuatilifu viligawanywa kwa akina mama na 5,000 vilinunuliwa na wananchi wenyewe. Ugonjwa wa vikope umepungua kwa 1%. 99% ya watoto walio chini ya miaka 5 walipata matone.

 

Mfuko wa afya unafanya kazi na hadi sasa una jumla ya wanachama 18,574. Lengo letu ni kuongeza idadi ya wanachama hadi kufikia 30,000 ifikapo mwaka 2010. Kiasi cha shs.92,000,000/= zimeshachangwa. Baada ya kupokea mchango wa serikali mfuko una kiasi cha shs. 187,223,535/=. Wanachama wa Bima ya Afya wameongezeka hadi kufikia 12,200.

 

Juhudi za kuhamasisha zinaendelea ili kila kaya iweze kujiunga na kuwa Wanachama wa Mfuko wa Jamii ili waweze kupata huduma hii ya Afya kwa urahisi.

Tunahakikisha kuwa madawa muhimu yanapatikana kwenye vituo.

Watumishi 30 wa afya walipewa mafunzo ya utambuzi wa magonjwa ya moyo.

Ukimwi

Kiwango cha maambukizi kinakadiriwa kuwa 1.4% Watu 6,500 wanaishi na virusi vya UKIMWI.  Mikakati ya Wilaya ya mapambano ni uhamasishaji ngazi zote, wenye virusi vya UKIMWI  wanaelimishwa  umuhimu wa kuhudhuria kliniki kupata dawa na ushauri nasaha, na mafunzo kwa kamati za kudhibiti UKIMWI ngazi ya kata na vijiji.

Lengo letu ni kupunguza maambukizi mapya na kuhamasisha jamii kupima afya mara kwa mara.

Mafanikio ni mwitikio mzuri na ushirikiano chanya tunaoupata kutoka taasisi za dini. Wadau wanaohusishwa katika kutekeleza azma hii ni pamoja na KIWAKUKI, KINSHAI, CHAKUWAYA, KIKUURO na RCC.

Mbinu zinazotumiwa na Wilaya kupambana na UKIMWI

Kuanzisha Kamati shirikishi za kuthibiti UKIMWI kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji na Wilaya.

UKIMWI umekuwa ajenda ya kudumu kwenye mikutano katika ngazi mbali mbali hapa Wilayani.

Kuhamasisha na kuimarisha upimaji damu wa hiari na kuendelea kutoa ushauri nasaha kwa Jamii.

Vituo vya kupima vimeongezeka toka 22 hadi 30.

Idadi ya wanaopima imeongezeka kwa 11%.

Watumishi  12 wamejengewa uwezo wa kutoa dawa za kurefusha maisha.

Vijana

Tuna vijana takriban 3,400 wasiokuwa na ajira za hakika.

Sensa ya kubaini mahitaji/stadi za vijana wetu imefanyika.

Wilaya ina mtandao wa mafundi – ROMBO DALTA wenye mafundi vyuma, useremala, uashi na cherehani.  Aidha kwa ushirikiano na SIDO, wilaya inajenga  Kombania ya Viwanda (Industrial Cluster) kwa lengo la kusaidia vijana wetu.  Tumeimarisha SACCOS kwa ajili ya vijana kupata mikopo ya biashara na uzalishaji mali.

Lengo la wilaya ni kuwawezesha vijana hawa waweze kujiajiri katika kilimo, ushonaji na ufundi.

Tumefanikiwa kuwezesha vijana 48 kufungua mashamba nje ya Wilaya.

Changamoto ni kuwawezesha vijana wengi zaidi kufungua mashamba nje ya Wilaya; na kuwapatia mafunzo ya ufundi wale wenye mwelekeo wa ufundi.

UTAWALA BORA

Wilaya ina Ofisi ya TAKUKURU inayoratibu na kusimamia mikakati ya kudhibiti rushwa. Mikakati hiyo ni pamoja na  kuainisha mianya ya rushwa, kuelimisha wananchi kuhusu haki zao  kupitia mijadala ya wazi, semina na mikutano.  Wananchi 1,812 wamepewa  elimu           hiyo na kutakiwa kutoa ushirikiano kudhibiti rushwa.  Aidha klabu 23 za wapinga rushwa zimeanzishwa na       zinaendelea            kwa    kupitia maigizo, nyimbo, ngonjera na mashairi.  Mashindano ya              insha na uchoraji katuni yanafanyika.

Mpango umeandaliwa wa kuimarisha utawala bora. Fedha za mishahara ya watumishi kwa kiwango kipya cha  mishahara zinalipwa ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Aidha waheshimiwa madiwani wamerekebishiwa viwango vipya vya posho zao.

            Fedha za mafunzo ya kuijengea uwezo halmashauri; watumishi na Waheshimiwa Madiwani zimetengwa.

Vijiji vyote 60 vitanunuliwa shajara kwa ajili ya kuongeza nguvu katika utekelezaji wa kazi za ofisi za vijiji.

            Imefanyika semina  kwa watu na  Waheshimiwa madiwani kwa kupitia Kamati zote za halmashauri.  Watumishi wote 2,275 wamepata semina kupitia vikao vya kila idara na pia kwa njia ya vipeperushi na kalenda toka ofisi ya TAKUKURU.

Wenyeviti na wajumbe wa Serikali za Vijiji wamepewa mafunzo kuhusu vita dhidi ya Rushwa.

Ratiba za vikao kwa mwaka mzima ziliandaliwa na zinafuatwa kwa ngazi zote.

 

HALI YA SIASA

Hali ya Wilaya kwa ujumla ni shwari kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita iliyopita. Makosa yaliyoripotiwa Polisi ni unyanganyi kwa kutumia nguvu, silaha, kujeruhi. Ili kukabiliana na ujambazi unaotusumbua mara kwa mara Wilaya iliunda Kombania za Mgambo kwa kila Tarafa kusaidiana na Polisi. Tunaendelea kuwajengea raia wetu uwezo nao wawe na ujasiri wa kutoa taarifa zozote wanazozijua kuhusiana na ujambazi na uhalifu kwa ujumla.

 VYAMA VYA KISIASA VIMEKUWA VIKIJISHUGHULISHA NA:

Kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Kufafanua sera mbalimbali za Serikali kwa wananchi.

Kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki katika kampeni mbalimbali za kitaifa km. Vita dhidi ya rushwa, maambukizi ya Ukimwi na shughuli za kujitolea.

UWAJIBIKAJI WA HALMASHAURI KWA WANANCHI (LLGAS)

Wananchi 87 walipata mkopo wa jumla shs.59,600,000.00 kupitia benki ya NMB na wamesharejesha jumla  sh.59,915,670 hadi Julai 2008.  Wananchi wengine 86 wamepata mkopo wa shs.150,425,000.00 kutoka benki ya CRDB kupitia Saccos za Motamburu na Nanjara Reha.  Nao hawa wamerejesha shs.116,045,054.00 hadi mwezi Julai 2008.

Mafunzo kwa watendaji wa kata 20 na VEOS 60 yamefanyika.

Mihtasari ya vikao vya ngazi zote imekaguliwa.

Mashirika ya dini na taasisi mbalimbali wameanzisha vituo vya kulelea watoto yatima, mfano: Ngaleku Orphan Centre na Huruma Tumaini Centre.

Jamii  imeelimishwa kuhusu madawa ya kulevya.

Walemavu wote wanashiriki katika chaguzi za ngazi zote kuanzia vitongoji, vijiji, kata, wilaya na zile za Kitaifa.

Vijiji vyote 60 vimeshiriki ujenzi wa shule za sekondari za kutwa hadi kufikia sekondari 34.

 

Idadi ya walemavu walioko wilayani imebainishwa ili waweze kuingizwa kwenye mpango wa Halmashauri.

Taarifa za mapato ya Halmashauri zinasambazwa katika ngazi za chini kwa kutumia mbao za matangazo na kwenye mikutano ya ngazi zote.

Kiasi cha shs. 18,000,000 kimetolewa kwa vijiji 60 kusaidia shughuli zao za maendeleo.

 

USHIRIKISHWAJI WA LLGAS KATIKA KUPANGA MIPANGO (O&OD)

Mafunzo ya O & OD yamefanyika kwa viongozi wa ngazi zote za serikali za mitaa tangu mwaka 2004/05.

Mipango ya miradi ya sekta zote huwa inaandaliwa na Kamati za O&OD zilizoko katika kila kijiji baada ya kujadiliwa na kikao cha serikali ya kijiji na kisha kufikishwa kwenye kikao cha WDC kwa kuratibiwa na baada ya hapo kuwasilishwa wilayani.

MIKUTANO YA KISHERIA KWENYE HALMASHAURI NA LLGAS INAYOPASWA KUFANYIKA

Viongozi katika ngazi za vijiji na vitongoji wamekuwa wakihimizwa kuitisha na kuhakikisha kwamba vikao vinafanyika na mikutano mikuu kama inavyotakiwa  kisheria. Katika vikao hivi wanahimizwakutoa taarifa ya mapato na matumizi na pia kuwaeleza ni hatua  gani zinazochukuliwa katika kuzipatia ufumbuzi kero/malalamiko yao.

Viongozi wa halmashauri hushiriki kikamilifu vikao/mikutano hii ili kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yakiwemo yale ya kitaalam na pia kuwaelimisha/kuwafahamisha juu ya haki zao za kimsingi kisheria, nk.

Utawala Bora

Vikao vyote vya Halmashauri vimefanyika kulingana na ratiba.  Mikutano ya halmashauri za Vijiji, Vijiji na Vitongoji inaratibiwa na Wilaya.  Vikao vya Halmashauri zinatangazwa na hutumia vipaaza sauti.  Vijiji vina sheria ndogo za kilimo, mazingira na afya.  Masanduku ya maoni yako maeneo mbalimbali na yanatumika.  Mahusiano kati ya viongozi na watendaji ni mzuri.  Aidha mahusiano baina ya Halmashauri na wadau wengine; mfano; asasi zisizo za serikali ni mazuri.

Viongozi ngazi za vijiji walipewa mafunzo kuhusu majukumu na wajibu wao.  Taarifa za mapato na matumizi hutolewa kwenye mikutano ya vijiji.  Mwenyekiti wa halmashauri huwwaeleza wananchi maendeleo na mafanikio ya Halmashauri kila mwaka.

 

HITIMISHO

Changamoto Zinazoikabili Wilaya

Kushuka kwa kipato cha wananchi wa wilaya ya Rombo. Pato la mwananchi wa Rombo linakadiriwa kuwa ni shs. 250,000/= kwa mwaka (DGDP Survey, 2007). Hii ni sawa na dola za Amerika 167 kwa mwaka. Dola 14 kwa mwezi au dola 0.5 kwa siku.

Zao kuu la biashara linazalishwa chini ya viwango vya kitaalam.Eneo lilimwalo kahawa lina uwezo wa kuzalisha tani 6,000 kwa mwaka. Ili kahawa hii ipate bei nzuri italazimu kuongeza ubora na wingi wake. Hii inapaswa kuanzia tangu kipindi cha matunzo shambani, namna ya umenyaji maganda, usafishaji hadi ukaushaji. Pamoja na yote haya yanahitajika madawa na mbolea zaidi na mashine za kumenya.

Msongamano wa watu ni mkubwa mno unaosababisha ufinyu wa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo. Watu wanalazimika kuzalisha mazao kwenye eneo dogo.

Mahitaji ya shule za sekondari ni makubwa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanomaliza elimu ya msingi. Tatizo hili linakuzwa kutokana na uhaba wa maeneo ya kujenga shule na huduma nyingine za jamii.