| MALIASILI | UVUVI | UTALII |  
   
Rudi nyumbani
   
................................................................................................................................. ................................................................................................................................. .................................................................................................................................
         
 
UTANGULIZI
 
 
 
Afisa Maliasili wa Mkoa
 
 
Mkoa wa Kilimanjaro umegawanyika katika Wilaya sita na Halmashauri saba. Mkoa una zaidi ya watu 1.4 milioni. Eneo la Mkoa ni kilometa za Mraba 13,209. Misitu na mapori inachukua kilometa za mraba 9,537. Hifadhi ya Mazingira inajumuisha Misitu, Mapori ya Wanyamapori na Maeneo ya uvuvi(Mabwawa na Maziwa).
 
2.RASILIMALI ZA MALIASILI
 
Rasilimali hizo ni kama Misitu, Pori la Akiba la Wanyama la Mkomazi, Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro Bwawa la Nyumba ya Mungu , Pori la akiba la Mkomazi, Bwawa la Kalimawe, Rasilimali hizi zinakabiliwa na uharibifu mkubwa kwa kuwa zinahitajika kwa jamii katika kuinua hali ya maisha yao. Hali hii inatoa changamoto kwa watendaji
 
2.1 MISITU NA UFUGAJI WA NYUKI
 
Mkoa wetu una misitu iliyohifadhiwa kisheria kwa madhumuni ya Hifadhi ya Ardhi, Maji na Mazingira na mali ghafi kwa ajili ya viwanda Misitu hiyo inasimamiwa na Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, kama vile Kahe, Rau, Kilimanjaro, Vumari, Kindoroko, Chome, Kamwenda, Gonja, Kwizu, Kiverenge,Koko hill,Chambogo.
 
Uvunaji wa mbao katika mkoa wetu hufanyika kwenye misitu ya Rongai na West Kilimanjaro kwa utaratibu uliowekwa na unaozingatia uvunaji endelevu. Mashamba ya miti katika Mkoa wetu yana uwezo wa kutoa malighafi kiasi cha meta za ujazo 49,000 kwa mwaka (Rongai 32,000, West Kilimanjaro 16,000 na Ukanda wa Nusu Maili Rombo 1,000).Malighafi hiyo ni kidogo sana kutokana na mahitaji hasa baada ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, Mkoa una zaidi ya viwanda 65 vya kupasua mbao.
 
Ufugaji Nyuki unaenda sambamba na uhifadhi wa misitu, kwani ufugaji wa nyuki hufanyika maeneo ya misitu na vichaka.
 
2.2 HIFADHI YA MLIMA KILIMANJARO
 
Hifadhi hii inajumuisha misitu ya ukanda wa Nusu Maili chini ya usimamizi wa Halmashauri za Wilaya ya Rombo, Hai, Moshi. Mashamba ya miti ya Rongai na West Kilimanjaro , Msitu wa Asili wa Hifadhi ya Ardhi na Maji (Catchment Forestry) na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro. Eneo hili humilikiwa na shirika la hifadhi za taifa,idara ya misitu na nyuki na Halmashauri za Wilaya ya Rombo, Hai na Moshi
 
Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kuweka Msitu wa Asili wa Hifadhi ya Ardhi na Maji chini ya usimamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA). Taratibu za kuifanya misitu hii kuwa sehemu ya Hifadhi za Taifa zinaendelea kufanyiwa kazi Wizarani.
 
2.3 HIFADHI YA MAZINGIRA
 
Upo uharibifu mkubwa unaofanyika hasa kwenye maeneo ya wenyeji ambapo kuna tatizo kubwa la kulima kwenye makorongo, miteremko mikali na kando za mito na matokeo yake ni mmomonyoko wa udongo . Hifadhi zilizokuwa kwenye maeneo ya mito zimebadilishwa kuwa maeneo ya Kilimo cha Mahindi na Migomba
 
 
Hali hii imepelekea Serikali kutoa Tamko mwaka 2006 kuhusu hifadhi ya Ardhi na Vyanzo vya maji.Katika Tamko kila wilaya ilitakiwa kutekeleza Tamko hilo na kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika.Hata hivyo Serikali kwa mwaka huu imetoa fedha kwa ajili ya UDEM kwa kila wilaya kwa maana ya kujenga uwezo wa watendaji, hivyo tutumie nafasi hiyo kuona kuwa sekta ya maliasili inaweza kutimiza wajibu wake kwa kutumia rasilimali hizo.
 
Mafanikio ya mradi wa UDEM, TASAF NA USIMAMIZI SHIRIKISHI WA MISITU (PFM) itajibu maswali mengi kuwa sekta hiyo ilikuwa haipewi rasilimali.
 

2.4 HIFADHI YA WANYAMAPORI LA MKOMAZI

 
Pori Pekee la akiba la wanyamapori katika mkoa wetu ni Mkomazi .Pori hili limekuwa likipata matatizo kutokana na wachungi kuingilia eneo hilo kwa muda mrefu na kuchoma moto.Hata hivyo Wilaya na mkoa umepeleka mapendekezo Wizara ya Maliasili na Utalii ili kupandisha hadhi na kuwa Hifadhi ya Taifa.Wizara inakamilisha taratibu za kupandisha pori hilo kuwa hifadhi ya Taifa.
 

2.5 SEKTA YA UVUVI

 
Sekta ya Uvuvi hapa Mkoani nayo imeathirika sana kwani kutokana na ongezeko la watu, uvuvi haramu nao unafanyika zaidi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu. Hii inasababisha uvuvi wa samaki wadogo kabisa na kuangamiza mazalio ya samaki, na matokeo yake wananchi wa maeneo yenye shughuli za uvuvi wanaathirika sana na umaskini unazidi kuwaumiza, Maeneo makuu ya uvuvi katika mkoa wetu yalijulikana kama ziwa Jipe, Bwawa la Nyumba ya Mungu na Bwawa la Kalimawe.
 
Ziwa Jipe limevamiwa na magugu maji ambayo yanaelekea katika Bwana la Nyumba ya Mungu.Kushamiri kwa magugu maji ni matokeo ya kilimo kinachoendelea kwenye miteremko mikali ambayo husababisha mmomonyoko wa udongo ambao unapelekwa ziwani wakati wa mvua.
 
2.6 KUPAMBANA NA KUENEA KWA JANGWA MWAKA 2008/2009
 
Mwaka 1998 mkoa uliandaa mkakati wa upandaji miti kwa lengo la kupanda miti 5,000,000 kila mwaka kuanzia mwaka 1999/2000 hadi 2010/2011
 
BONYEZA HAPA kuona idadi ya miti iliyopandwa
 
3. CHANGAMOTO ZA MAZINGIRA MKOANI KILIMANJARO.
 
1. Ni kweli mkoa unazo rasilimali nyingi za maliasili ambazo kimsingi zinajulikana kwenye makaratasi lakini kuna upungufu mkubwa kuwa rasilimali hizo hazijulikani ziko kiasi gani hasa kutokana na ukosefu wa takwimu (upandaji wa miti na uvunaji wa mazao ya misitu kutoka kwenye General land)
 
2. Bwawa la nyumba ya mungu limeanza kujaa udongo kutokana na mmomonyoko wa udongo kwa sababu za kilimo na ufugaji sehemu za juu kuzunguka bwawa
 
 
3. Bwawa la nyumba ya mungu kuvamiwa na magugu maji kutoka Ziwa Jipe lililopo mpakani mwa Nchi ya Kenya na Tanzania.
 
 
4. Upungufu mkubwa wa mazao ya miti kutokana na ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, matumizi ya nyumbani hasa kwa wakazi wa mijini na uchomaji moto ovyo nyakati za kiangazi.kwa mfano pori la Mkomazi na Hifadhi ya Kilimanjaro.
 
5. Mtandao wa mawasiliano unachangia zaidi kwa wafanyabiashara kuendelea na biashara haramu
 
6. Ongezeko la watu wanaotegemea rasilimali hii isiyoongezeka kwa kasi sawa na ya ongezeko la watu.n.k.
 
7. Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Maliasili imetoa maelekezo mbalimbali na ratiba ya uhamasishaji wa upandaji wa miti na siku za mazingira duniani hivyo taarifa kama hiyo inapohitajika ipatikane kwa wakati katika format Ambayo imekuwa ikitumwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.angalia kiambatisho ya format hiyo.
 
8. Inaeleweka kuwa siku ya upandaji miti itatofautiana kwa kila wilaya kutokana na hali ya unyevu hivyo ni changamoto kwetu tukawa na ratiba zetu za ndani
 
 

4.MAPENDEKEZO

 
1. Katika kukabiliana na changamoto zilizoelezwa hapo juu na nyinginezo ni muhimu tukajiwekea mikakati ambayo itapimika na itatoa picha kamili kuhusu sekta ya maliasili kwa ujumla wake na mchango wake katika kupunguza umaskini katika jamii ya watanzania.
 
2. Ni muhimu kwa watendaji tukawa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa walengwa bila kutofautiana kati ya wilaya na mkoa (Hili linatokea hasa pale taarifa inapohitajika wizarani na wilaya husika kutotoa taarifa yake kwa wakati muaafaka) kwa mfano taarifa za upandaji miti na ratiba za maadhimisho ya wiki ya mazingira Duniani.
 
3. Elimu zaidi ya mazingira itolewe kwa jamii yote Mkoani hususan upandaji wa miti na ufugaji wa nyuki na samaki
 
4. Nguvu zaidi za dola na ushiriki wa jamii ni nyenzo muhimu zinazohitajika kuhakikisha kwamba uvunaji haramu unakabiliwa ipasavyo.
 
5. Viongozi wa Vijiji na Kata waelekezwe kuhusu wajibu wao kama viongozi kwani ushiriki wao ni mdogo katika kuwasaidia wataalamu wwanapotimiza wajibu wao
 
6. Kusaidia na kushauri kuanzisha miradi itakayomuongezea mwananchi kipato kwa kutumia ujuzi wake na mazingira yake Mfano ufugaji nyuki.
 
7. Kamati za mazingira za vijiji, kata na wilaya zifufuliwa na ikibidi ziwezeshwe kwa kuwapatia mafunzona majukumu yao.na utekelezaji wa majukumu yao ufuatiliwe.
         
Rudi juu   Rudi juu   Rudi juu
 
.........................................................................................................................................................................................................................................................................................
 
COPYRIGHT© OFISI YA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO, S.L.P 3070, SIMU: 027 2752184/54236-7, FAX: 027-2753248. HAKI ZOTE ZIMEHIFADHIWA.