Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeendesha mafunzo maalum kwa Maafisa Utamaduni na Maafisa Biashara kutoka Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu matumizi ya mifumo ya kidigitali ya AMIS na TAUS, ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 14 na 15 Mei 2025 yamelenga kuwawezesha watendaji hao kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi zaidi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali linalotaka mifumo yote ya kielektroniki iwe imeunganishwa ifikapo Desemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mafunzo hayo, Afisa TEHAMA wa BASATA, Bw. Octavias Bagaye alisema kuwa kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutarahisisha utendaji kazi na kuboresha huduma kwa wasanii, wakiwemo wale wanaojisajili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa na Maonyesho kutoka BASATA, Bi. Lilian Shayo ametoa wito kwa wasanii na wadau wa sanaa Mkoani Kilimanjaro kujisajili kupitia kwa Maafisa Utamaduni katika halmashauri zao ili kurasimisha kazi zao na kufaidika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia BASATA katika kuhakikisha sekta ya sanaa nchini inakuwa kwa kutumia teknolojia na mifumo ya kisasa.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa