Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya mabasi mawili kugongana na baadaye kushika moto wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, imeongezeka na kufikia 42, kutoka 39 vilivyoripotiwa awali.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Julai 2, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kuwa kati ya waliopoteza maisha, 31 walikuwa wakisafiri katika basi dogo aina ya Coaster, huku wengine 11 wakiwa kwenye basi kubwa.
Kuhusu hali ya majeruhi, mkuu huyo wa mkoa amesema jumla ya watu 24 waliokuwa wamelazwa tayari wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali zao kuimarika, huku majeruhi wawili wakiendelea kupokea matibabu hospitalini.
Aidha, Mhe. Babu amesema Mkoa tayari umeshapokea majibu ya vipimo vya vinasaba kutoka kwa mkemia Mkuu wa Serikali mapema leo tarehe 02 Julai 2025, hivyo zoezi la kukabidhi miili ya marehemu kwa ndugu na jamaa litafanyika siku ya Alhamisi tarehe 03 Julai 2025 katika hospitali ya Rufaa ya KCMC. Ambapo Serikali inatarajia kukabidhi jumla ya miili 36 kwa wanafamilia husika ili kuweza kuendelea na taratibu za mazishi. Gharama za majeneza, Sanda na kusafirisha miili ya marehemu zitagharamiwa na Serikali kwa kutoa kiasi cha fedha kwa kila familia ili kufanikisha mazishi ya wenzetu hao.
Aidha maziko ya miili sita (6) ya wenzetu ambao wao walitambulika kirahisi na kutohitaji DNA yalifanyika tarehe 30 Juni, 2025.
Amesema katika ajali hiyo hadi kufikia leo jumla ya watanzania wenzetu 42 wamefariki ambapo 31 (ikiwa ni wanawake 21 na wanaume 10) walikuwa kwenye coaster na 11 (ikiwa ni wanawake 7 na wanaume 4) walikuwa kwenye basi la channel one. Aidha, majeruhi waliopatikana katika ajali hii ni 28 ambapo kati yao 13 ni wanaume na wanawake 15. Majeruhi wote hao waliendelea kupata matibabu katika Hospitali zetu ikiwa ni pamoja na hospitali ya Wilaya ya Same, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda (KCMC) ambapo kati ya majeruhi hao, majeruhi 24 wameruhusiwa, wawili (2) wameaga dunia wakati katikati ya matibabu na wawili (2) waliobaki wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda (KCMC) na Hospitali ya Wilaya ya Same.
mnamo tarehe 28 Juni, 2025 majira ya saa 11 jioni, mkoa wetu ulipata tukio la ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Saba Saba, Kitongoji cha Mahuu, Kata ya Same takriban kilomita 4 kutoka Same Mjini, Wilaya ya Same – Mkoa wa Kilimanjaro ikihusisha basi kubwa la abiria lenye usajili wa namba T-179 la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Arusha kuelekea Tanga na Coaster ya abiria yenye namba za usajili T-199 EFX inayomilikiwa na kampuni ya MWAMI TRANS iliyokuwa ikitokea Same kuelekea Manispaa ya Moshi.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa