Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Kiseo Nzowa pamoja na viongozi wengine wameshiriki zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Kilimanjaro Manispaa ya Moshi ambapo zoezi hilo limeanza rasmi Disemba 11 hadi 17, 2024 Mkoani hapa.
Mhe.Nurdin Babu ametoa pongezi kwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa kazi nzuri ambayo wameanza kufanya katika Mkoa wa Kilimanjaro na kusema kuwa Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa Mikoa ambayo imeanza kufanya uboreshaji wa daftari la mpiga kura kwa mwaka huu wa 2024, aidha amesema zoezi hili la uboreshaji wa taarifa ni muhimu sana kwa wananchi wote na Watanzania kwa ujumla.
“Ndugu wananchi zoezi hili la uboreshwaji wa taarifa ni la muhimu sana katika nchi yetu kwahiyo leo mimi pamoja na viongozi wenzangu na nyinyi wananchi tumejitokeza kwa wingi kuja kuboresha taarifa zetu”
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kufanya maboresho ya taarifa zao ili ifikapo Oktoba 2025 waweze kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Nipende kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa huu mjitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zenu ili ifikapo uchaguzi Mkuu 2025 muwe na kibali na haki ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wa nchi yetu pia kwa wale ambao wanakaribia kufikisha umri wa miaka 18 wafike kwenye vituo ili wapewe maelekezo na viongozi wa Tume Huru ya uchaguzi ili na wao waweze kujiandikisha” Amesema Babu
Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bi.Mwajuma Nasombe ametaja makundi yanayotakiwa kwenda kufanya uboreshaji wa taarifa zao, ambao ni wale watakao timiza umri wa miaka 18 kabla ya tarehe ya uchaguzi Mkuu 2025 ,wale waliojiandikisha awali na kuama Kata au Jimbo kwenda maeneo mengine, wale wenye taarifa zilizokosewa wakati wa uandikishaji hapo awali na wale waliopoteza kadi zao ya kupiga kura au wenye kadi zilizo aribika.
Kwa upande wake Mratibu wa uandikishaji Mkoa Bw. Jasper Ijiko amesema kuwa “tumejipanga vema kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa na jambo kubwa la mahususi kwa kushirikiana na Tume Huru ya Uchaguzi ni kuendelea kutangaza na kuhabarisha wananchi wale wote wenye sifa tunatarajia wananchi wote hadi kukaribia tarehe 17 Disemba 2024 watakuwa wamejiandikisha katika vituo vipatavyo 1300 katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa