SIKU saba za nderemo, shamrashamra, mshike mshike, na mapokezi ya kihistoria zilishuhudiwa mkoani Kilimanjaro kuanzia Juni 28 hadi Julai 5 mwaka huu, wakati Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2025 ulipowasili na kukimbizwa katika halmashauri zote saba mkoani humo.
Kauli mbiu ya mwaka huu “Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu 2025, kwa Amani na Utulivu” ilisikika kila kona ya mkoa, ikiwaalika Watanzania kushiriki mchakato wa kidemokrasia kwa hali ya utulivu na mshikamano.
Katika mapokezi ya Mwenge huo wa Uhuru kutoka mkoa wa Kaskazini Pemba hadi Kilimanjaro, na hatimaye kuukabidhi mkoani Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, alitangaza mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia mbio hizo zenye lengo la kuhamasisha maendeleo, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza katika kijiji cha Kingori, kata ya Malula wilayani Arumeru, alipokuwa akikabidhi Mwenge huo Julai 5, Mhe. Babu alisema Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa jumla ya kilomita 895, ambapo miradi 52 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 84 ilikaguliwa, kuzinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi.
“Mkoa wa Kilimanjaro tulipokea Mwenge huu kwa moyo wa uzalendo na kazi. Tumezindua miradi 22, kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 20, na kutembelea miradi 10. Yote imepokelewa vizuri na imeridhisha,” amesema Babu
Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali
Katika kuonyesha mshikamano wa sekta binafsi na serikali, miradi 9 ya kijamii ilitembelewa ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za maendeleo ya wananchi. Pia, mkoa uliendelea kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa mitungi 370 ya gesi safi kwa matumizi ya kupikia yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 18.4, ikiwa ni hatua ya kulinda mazingira na afya za wananchi.
Katika upande wa afya, zaidi ya watu 1,800 walijitokeza kupima VVU, ambapo waliobainika kuwa na maambukizi ni 12 tu sawa na asilimia 0.67 na Damu salama iliyopatikana ilikuwa unit 177, huku waliopima malaria wakiwa 812 bila kubainika na maambukizi.
Kupitia elimu ya rushwa na miongozo ya TAKUKURU, jumla ya kesi 401 ziliripotiwa, ambapo kesi 201 zilikuwa na viashiria vya rushwa na kesi 20 zilitolewa hukumu
Pia katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, watuhumiwa 555 walikamatwa, kesi 232 zipo mahakamani, na kesi 106 tayari zimepewa hukumu.
Mshikamano wa Viongozi na Askari
Kiongozi wa mbio za Mwenge Taifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, alisifu kwa dhati uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, hasa Wakuu wa Wilaya na Kamati za Usalama kwa usimamizi madhubuti.
Aliwapongeza pia askari wa FFU mkoani wakiongozwa na ASP Frank Agapiti kwa ulinzi imara usiku na mchana,na akimuomba RPC Simon Maigwa kuwapa mapumziko ya siku 6-7 pamoja na posho ya kujikimu kutokana na kazi kubwa waliyoifanya.
“Niombe kwa dhati kabisa, viongozi hawa waliopo hapa mkoa wa Kilimanjaro wasiondoke. Rais wetu mpendwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahitaji watu wa aina hii. Wameonyesha weledi, uzalendo na ufanisi mkubwa sana,” alisema Ussi kwa msisitizo.
Uratibu Bora wa Irene Kiata Mratibu wa Mwenge
Kwa upande wa maandalizi ya kitaalamu, kiongozi huyo alimtaja Bi. Irene Kiata, Mratibu wa Mwenge wa Uhuru kimkoa na timu yake kuwa miongoni mwa waratibu bora aliowahi kufanya nao kazi.
Alieleza kuwa utulivu na usikivu wao ulirahisisha kazi ya timu ya taifa kufanya kazi kwa mafanikio makubwa.
“Nitamuomba Rais Dkt. Samia, kuwatunuku vyeti waratibu 10 bora wa kimkoa mwaka huu ifikapo octoba 14 mwaka huu na pia akuangalie kwa jicho la pekee katika majukumu unayofanya ” alisema Ussi
Mwenge Wapita Kila Kona ya Mkoa
Mwenge wa Uhuru ulipita katika halmashauri zote saba: Manispaa ya Moshi, Moshi DC, Hai, Siha, Rombo, Mwanga na Same.
Manispaa ya Moshi peke yake, ilikimbizwa kwa kilomita 53.5 ambapo miradi 7 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 13.5 ilizinduliwa, ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Matunda, mradi wa maji Karanga Darajani, ujenzi wa hoteli ya kisasa, na soko jipya la mboga Mbuyuni.
Moshi Vijijini, Mwenge ulikimbizwa kwa kilomita 69.9, ukitembelea miradi 8 ya bilioni 1.9, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, mradi wa siagi ya karanga kwa vijana na daraja la Mikameni.
Katika Wilaya ya Same, Mwenge ulikimbizwa kilomita 102.3, ukizindua miradi ya bilioni 2 ikiwemo zahanati, barabara, na mradi wa maji Mroyo–Kizangaze.
Wilaya ya Mwanga ilipokea Mwenge kwenye miradi 8 ikiwemo ujenzi wa bweni, zahanati, kisima cha maji, na daraja la Mandaka-Izungo. Jumla ya gharama ya miradi hiyo ilikuwa zaidi ya bilioni 1.1.
Katika Wilaya ya Rombo, miradi 7 ya thamani ya bilioni 3.7 ilihusishwa, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, nyumba za watumishi, na mradi wa maji Enduiment.
Wilaya ya Siha ilikimbiza Mwenge kwenye miradi 8 yenye thamani ya bilioni 4, ikiwemo shule mpya ya Sekondari, mradi wa maji Gararagua, na ufugaji wa kuku wa kibiashara.
Hai, Mwenge ulikimbizwa kwa kilomita 90, ukipitia miradi 7 ya zaidi ya bilioni 3, ikiwemo ujenzi wa jengo la OPD, barabara ya lami, mradi wa maji wa Kikafu Soka, na jengo la biashara.
Aidha tukio la Mwenge wa uhuru 2025 limeacha alama ya maendeleo ya kweli mkoani humu na ni ushahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kwa kusogeza huduma kwa wananchi.
Kwa hakika, Mwenge wa Uhuru si tu alama ya historia ya ukombozi wa Taifa letu, bali pia ni dira ya maendeleo, mshikamano na uzalendo.
Mkoa wa Kilimanjaro umeandika historia ya kipekeea mshikamano wa viongozi, wananchi, askari na timu ya uratibu.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa