Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro imetoa Msaada kwa Wanawake Waliojifungua na Watoto Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi,ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani,Machi 8,Mwaka huu.
Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Mkoa Nurdin Babu amesema kwamba msaada huu ni ishara ya upendo na kujali kwa wanawake hao na watoto wao, akisisitiza kuwa ni muhimu kuwaunga mkono katika nyanja mbalimbali za maisha, hasa katika kipindi hiki cha maadhimisho ya wanawake.
Kwa upande wake, kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, Jonas Kessy, amesema kuwa vifaa walivyokabidhiwa vitasaidia kuboresha huduma kwa wanawake na watoto wao. Kessy alieleza kuwa hospitali hiyo itahakikisha vifaa hivyo vitatumika ipasavyo ili kusaidia katika maendeleo ya wamama na watoto hao.
Miongoni mwa misaada iliyotolewa ni pamoja na taulo za kike, sabuni za kufulia, na pampasi, vifaa ambavyo vinatarajiwa kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto katika hospitali hiyo.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ameshiriki pia katika zoezi la upandaji miti katika Shule ya Msingi Mshikamano, iliyopo kata ya Boma Mbuzi, Manispaa ya Moshi. Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuwajengea jamii dhamira ya kupenda mazingira.
Huu ni mfano mwingine wa juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro katika kuhakikisha maendeleo ya jamii na mazingira yanapewa kipaumbele.
Hadi kufikia tarehe 8 Machi, mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanaendelea, huku wanawake na watoto wakikumbukwa na kutolewa msaada mbalimbali ili kuboresha hali zao.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa