Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameushauri uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini TAKUKURU kuanza utaratibu wa kutoa mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa watumishi wake ili kuwajengea uwezo zaidi wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Simbachawene alitoa ushauri huo Mei 15, 2023 Mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa waajiriwa wapya wa TAKUKURU yanayofanyika kati Shule ya Polisi Tanzania (TPS).
"Watumishi wa TAKUKURU wanafanyakazi ya kuchunguza maswala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo; kwa sasa kuna wale ambao wanatumia teknolojia ya kisasa kufanya uhalifu ikiwemo ubadhirifu wa fedha hivyo kwa kupata mafunzo haya mtakuwa mmewaongezea uwezo katika kutekeleza majukumu yao", alisema.
Aliongeza, "Ni vyema somo la elimu ya IT likafanywa la lazima kwa kila anaeajiriwa na taasisi hii kwani uhalifu wa kimtandao haswa ule ambao TAKUKURU hutumia kukabiliana nao hufanywa kwa kupitia mitandao; mtumishi hawezei kufanya uchunguzi wa uhalifu wa aina hii bila kuwa utalaam wa IT".
Aidha, alitoa rai kwa uongozi wa TAKUKURU kuendelea kushirikiana na taasisi zingine likiwemo Jeshi la Polisi katika kupambana na rushwa hapa nchini haswa ikitiliwa maanani ya kuwa mpaka mtu afikirie kutumia rushwa huwa tayari ashafanya njama nyingi.
Mhe. Simbachawene aliendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa taasisi hiyo ili kuhakikisha inafanikiwa katika kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya Taifa haswa ikitiliwa maanani Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo na ambazo ni lazima matumizi yake yaonekane yanaenda na fedha halisi.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Rashid Salum Hamdun, alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa na inaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake.
"Kwa mfano ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dr Samia, Serikali imetoa kibali cha kuajiri jumla ya watumishi wapya 700 ambao ni sawa na robo ya watumishi wote ambao wamejiriwa na taasisi hii tangu inanzishwe mwaka wa 1975 wakati huo ikijulikana kama PCB", alisema na kuongeza, huu ni mchango mkubwa sana kwa PCCB katika kutekeleza majukumu yake.
Kuhusu mafunzo hayo, ACP Hamdun alisema kuwa ambao kabla ya kuteuliwa kwao kujiunga na taasisi hiyo kulifanyika vetting ya hali ya juu.
"Zilipotangazwa nafasi hizi, uongozi wa taasisi ulipokea maombi takribani 33,000 na baada ya usahili walipatikana 320 ambao ndiyo wanaanza mafunzo yao leo", alisema.
Alisema mafunzo hayo ni ya lazima kwa kila mtumishi aneajriwa na taasisi hiyo, ambapo alisema wahusika hao watapata mafunzo ya kinadharia na vitendo, ambayo alisema yatahusisha pamoja na elimu nyingine, ile ya uchunguzi wa jinsi ya kutambua na kupambana na vitendo vya rushwa.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babau aliwaasa wahusika wa mafunzo hayo kuhakikisha wanaweka uzalendo mbele wakati wakitimiza wajibu wao kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.
"Uzalendo ndiyo silaha ya kwanza na muhimu kabisa katika mapambano dhidi ya rushwa; Tanzania itapata maendeleo ya kweli na kuendelea kupata heshima duniani kote iwapo mtazingatia uzalendo wakati wakutekeleza majukumu yenu haswa katika kufuatilia miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa na fedha nyingi zinazotolewa na Serikali yetu", alisema.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa