Watumishi wa umma katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (mawenzi) wameagizwa kuwaelimisha wananchi juu ya haki zao za kisheria na kisera hususan misamaha ya uchangiaji wa gharama za matibabu kwa wazee, wajawazito na watoto.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea mwenendo wa utoaji wa huduma kwa wanannchi katika hospitali hiyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Mhe.Mghwira amesema miongoni mwa changamoto alizozigundua ni pamoja na baadhi ya wanufaika wa misamaha ya uchangiaji wa gharama za matibabu kutojua kuwa wana haki ya kupata matibabu pasipo kuchangia gharama.
Kuhusu wagonjwa wenye sifa za misamaha ambao wamepatwa na dharula mbalimbali ikiwemo kutobeba vielelezo vya misamaha hiyo, Mhe. Mghwira amewataka watoa huduma hao kuweka kipaumbele kwenye kuokoa maisha ya watu baada ya hapo zifuatwe taratibu za kupata vielelezo ili wapate misamaha.
"Kama mzeee ameshafika hospitali akiwa na hali mbaya lakini amesahau kadi yake ya msamaha wa uchangiaji wa huduma asirudishwe nyumbani, hakikisheni mnamhudumia kwanza huku mkifanya juhudi za kupata uthibitisho wa msamaha wake." alisema Mhe. Mghwira.
Kwa upande wake katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Aisha Amour ameuagiza uongozi wa hospitali kuweka mabango yanayotoa elimu kwa makundi yaliyopewa msamaha ili iwarahisishie kujua waende wapi ili wapate huduma kwa mujibu wa sheria na miongozo ya serikali.
Ameongeza kuwa endapo mabango hayo yatachakaa yawekwe mengine iwezekanavyo ili wananchi hao wasihangaike katika kupata huduma hizo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Mkoa Jonas Mcharo ameahidi kufanyia kazi maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa