MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO AHUDHURIA MAZISHI YA WAATHIRIKA WA AJALI WILAYANI MWANGA
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, ameshiriki ibada ya kuwaaga baadhi ya miili ya waathirika wa ajali ya gari iliyotokea tarehe 3 Aprili mwaka huu katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya Mvungi lililokuwa likisafiri kutoka Ugweno kuelekea Dar es Salaam, ambapo liliteleza, kuacha njia na kuanguka bondeni, na kusababisha vifo vya watu kadhaa pamoja na majeruhi.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mheshimiwa Babu aliwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameeleza masikitiko yake kufuatia msiba huo mzito, na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wananchi, hasa wakati wa majanga, kwa lengo la kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza.
Aidha, Mheshimiwa Babu alieleza kuwa serikali itagharamia usafiri wa kusafirisha miili ya marehemu kwenda katika maeneo yao kwa ajili ya maziko.
Katika salamu zake, alitoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa waangalifu zaidi hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi, ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuzuilika.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa