Historia imeenda kuandikwa kwa mara ya tatu baada ya Mwenge wa Uhuru 2024 pamoja na Bendera ya Taifa kupandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu chini ya kikosi cha Jeshi la Wananchi la Tanzania
Zoezi kama hili mara ya mwisho kufanyika ni mwaka 2011 ambapo ilikuwa ni mara ya pili Mwenge huo kufikishwa katika kilele hicho.
Mwenge wa Uhuru ulizimwa octoba 14,2024 jijini Mwanza baada ya kukimbizwa kwa siku 195 katika nchi nzima ambapo Rais Samia Suluh Hassan aliagiza upandishwe Mlimani Kilimanjaro ikiwa ni miaka 60 tangu uanze kukimbizwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Tanzania inapeleka Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro ili kuitangazia dunia kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni imara na pia itaendelea kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Aidha, Waziri Ridhiwani Kikwete amesema kuwa kwa mwaka huu 2024, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamuru Mwenge wa Uhuru upelekwe kilele cha Mlima Kilimanjaro baada ya kuhitimisha mbio zake kwa siku 195.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo Oktoba 15, 2024 katika hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wakati wa hafla ya kupokea kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambacho kimepewa jukumu la kupeleka Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa la Tanzania kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Vile vile, Waziri Ridhiwani Kikwete amehamasisha vijana kuendelea kuenzi falsafa za Mwenge wa Uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961.
Awali akizungumza, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema kupandishwa Mwenge wa Uhuru Mlima Kilimanjaro mwaka huu 2024 kunaleta hamasa ya uzalendo kwa wananchi hususani wakati huu ambao Tanzania inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru na mafanikio ya Taifa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia Mwenge wa Uhuru kupandishwa kwa mara nyingine katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Kiongozi wa kikosi Maalum, Luteni Kanali Khalid Hamisi amemhakikishia Mhe. Waziri Ridhiwani Kikwete kuwa kikosi hicho kitafikisha na kinaulinda na kuutunza Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa la Tanzania hadi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa