Halmashauri Mkoani Kilimanjaro zimetakiwa kuhakikisha zinatenga asilimia 10 kwa wakati kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Aliyasema hayo wilayani Rombo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai katika kikao cha Baraza Maalum la Madiwani cha kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Alisema ni wajibu wa kila halmashauri kufuata kanuni namba 5.5(1)ya Sera ya Mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2019 lengo likiwa ni kusaidia ukuzwaji wa mwananchi mmoja moja na taifa kwa ujumla.
"Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani anamatamanio makubwa sana ya nchi hii kusonga mbele, lakini haiwezi kusonga mbele bila kufanya kazi, hivyo naagiza fedha hizo zitolewe ili kwenda kuinua wananchi kiuchumi hasa yale makundi yaliyoelekezwa, Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu''.
Wakati huo huo Mhe. Kagaigai aliwataka wananchi wa mkoani hapa, kuchukua taadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona (COVID -1 9) huku akisema ni wajibu wa kila mmoja kwa mujibu wa taratibu za Wizara ya Afya.
Alisema kuwa ugonjwa huu upo lakini haipaswi kuchukuliwa kwa hofu bali ni kwa taadhari kama yalivyo magonjwa ya malaria kwa kuweka chandarua .
"Ugonjwa huu upo na ningependa wananchi tuendeleze utamaduni wetu tuliokuwa tunaufanya awali wa kunawa mikono mara kwa mara, kupaka vitakasa mikono na kuvaa barakoa pale mnapokuwa kwenye mikusanyiko, na uzingatie umbali wa kutosha kwa mujibu wa Wizara ya Afya".
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rombo Kanali Hamis Maiga akiwa kwenye Baraza Maalum la Madiwani Wilayani humo aliwataka madiwani kuongeza ushirikiano na watendaji ili waweze kupata matokeo bora katika halmashauri hiyo.
Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Serikali za Mitaa Grace Makiluli, amewataka Watendaji kuhakikisha wanazingatia na kutekeleza hoja zote zinazotolewa na Mkaguzi ili waweze kubaki na hati safi.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa