RC KILIMANJARO ATAKA WATUMISHI WA UMMA KUTII SHERIA NA KANUNI ZA KAZI
Serikali katika Mkoa wa Kilimanjaro imewataka watumishi wa umma kuendelea kutii sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika maeneo yao ya kazi, ili kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tarehe 1 Mei, 2025. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Babu alieleza kuwa baadhi ya watumishi wamekuwa na tabia zisizofaa kazini, ikiwemo kuchelewa kazini, kutoroka bila ruhusa na matumizi ya vileo, akiwataka waache mara moja na wajikite kutimiza majukumu yao kwa weledi na uadilifu.
"Baadhi ya wafanyakazi hawafanyi kazi ipasavyo. Unakuta saa tisa na dakika 28 tayari mtu anaondoka, anataka saa tisa na nusu awe ameshatoka getini. Huu sio utaratibu mzuri wa kuwatumikia wananchi," alisema Mhe. Babu.
Katika hatua nyingine, RC Babu aliwataka waajiri wote mkoani hapa kuacha mara moja vitendo vya unyanyasaji kwa watumishi, ikiwemo kuwapa majukumu nje ya muda wa kazi bila malipo na kuwazuia kuunda au kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
Aidha, aliwapongeza viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuendelea kusimamia maslahi ya watumishi katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Kiseo Nzowa, aliwataka watumishi wote wa umma kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu ili waache alama nzuri zitakazowakumbusha pale watakapomaliza muda wao wa utumishi.
Naye Katibu wa TUCTA Mkoa wa Kilimanjaro Ndg.Jackson Nyanganilwa alipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watumishi na kutatua changamoto zao kwa wakati.
Maadhimisho hayo yaliambatana na kauli mbiu isemayo: "Uchaguzi wa Mwaka 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali na Kuthamini Maslahi ya Wafanyakazi," ambapo pia watumishi hodari kutoka taasisi mbalimbali mkoani Kilimanjaro walitunukiwa zawadi kwa kutambua mchango wao katika utumishi bora.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa