Taasisi zote za Umma zilizopo Mkoani Kilimanjaro zimeelekezwa kulinda maeneo yao ili kuruhusu zoezi la anuwani za makazi kufanyika kwa urahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai ametoa maelekezo hayo februari 22, 2022 wakati wa uzinduzi wa anuwani za makazi lililofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuzindua anuwani katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, na kuweka kibao cha anuwani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, sheli ya PUMA na nyumba 2 za makazi za wananchi wa Manispaa ya Moshi.
Mhe. Kagaigai amesema watendaji wa taasisi wanatakiwa kuwa makini kwenye kulinda maeneo yao wanayoyamiliki kihalali ili kufanya uwekaji wa anuwani za makazi kufanyika kwa wepesi na hivyo itapelekea kuepusha migogoro ya ardhi na wananchi.
Ameendelea kusema baadhi ya taasisi zimekua zikiingia kwenye migogoro ya ardhi na wananchi ambao wamekuwa wakivamia maeneo yao na wengine kupelekea kujenga nyumba za kudumu.
Aidha, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Willy Machumu amesema Wakuu wa Taasisi watapelekewa sampuli za anuwani za makazi zenye maelekezo husika katika ofisi zao wakati huo watumishi wa Manispaa ya Moshi wanaofanya zoezi hilo la uwekaji wa anuwani wataweka alama kwa kutumia chaki huku mchakato wa vibao vyenye ubora na viwango vilivyopangwa ukiendelea kuandaliwa kwa ajili ya kubadikwa.
Akiwasilisha taarifa ya uzinduzi wa anuwani za makazi Mratibu wa zoezi hilo Mkoa Bw. Richard Emily amesema zoezi hili limetokana na changamoto zilizojitokeza katika Posta na anuwani za makazi ambapo masanduku ya posta yako 143,000/= nchi nzima ambayo ni idadi ndogo ukulinganisha na idadi ya wananchi kwa sasa. Amesema anuwani za makazi zinaundwa na vitu vitatu ambavyo ni namba ya nyumba au jengo, jina la barabara au mtaa na namba ya posti codi. Post codi ni namba maalumu inayotambulisha kanda,mkoa,wilaya na Kata.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo aliyeshika nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi amesema wilaya zinaendelea na zoezi la uwekaji wa anuwani za makazi ambapo wanaendelea kutoa ushirikiano wakutosha na kusimamia kwa weledi zoezi hilo pia kutumia muda uliopangwa kuhakikisha zoezi linakamilika kwa wakati.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa