Viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamehimizwa kutumia matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Wito huu umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu wakati wa ufunguzi wa Semina ya Usambazaji na Uhamasishaji wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Viongozi, Watendaji na Wadau wa Mkoa wa Kilimanjaro iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa CCP Oktoba 2,2023.
Mhe. Kasilda amesema mipango ya maendeleo izingatie matokeo ya Sensa na mwenendo wa kasi ya ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Kilimanjaro hasa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo Elimu,Afya,Maji,na barabara.
“Sisi kama mkoa wa Kilimanjaro tumeshaanza kutumia matokeo ya Sensa 2022 katika kupanga miradi ya maendeleo kwa wananchi wetu” amesema Mhe. Kasilda.
Ameongeza kuwa, semina hii itawajengea uwezo viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kutumia matokeo ya Sensa kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi katika ngazi zote za utawala.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imejipanga kuhakikisha matokeo ya Sensa 2022 yanawafikia wadau wote katika Nyanja mbalimbali ili yaweze kutumika katika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Dkt. Chuwa amesema, NBS inaendelea kuchakata matokeo ya Sensa 2022 ili kutoa takwimu nyingi zaidi zitakazokidhi mahitaji ya Serikali na wadau wa maendeleo.
“Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kuyasambaza matokeo ya Sensa kwa wadau wote ili yatumike kuwaletea wananchi maendeleo. Leo hii tupo hapa Kilimanjaro ili viongozi wa Kilimanjaro, wadau na wananchi wajue takwimu za mkoa wao na wazitumie kujiletea maendeleo” amesema Dkt. Chuwa.
Naye Kamisaa wa Sensa Mhe. Anne Makinda amesema Sensa 2022 imefanyika kwa mafanikio makubwa na sasa ni wakati wa kufaidika na matunda ya Sensa kwa kuyatumia matokeo hayo kuleta maendeleo.
Aidha, amesema watanzania aslimia 99.99 walihesabiwa na kufanya Sensa 2022 kuwa ya kihistoria na iliyopata uungwaji mkono mkubwa na wanachi na wadau wote ndani na nje ya nchi.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda amesema atahakikisha mipango yote ya Mkoa na bajeti inayokwenda kupangwa kwa mwaka wa fedha ujao itazingatia takwimu halisi za Sensa ya mwaka 2022 katika maeneo yote ya halmashauri saba za Mkoa kwa kuxingatia mipango ya fursa na maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa