Taasisi Mkoani Kilimanjaro zikiwemo TANROADS, TARURA, TFS na zingine zimeelekezwa kuuga mkono juhudi za kubadilisha Mkoa kuwa wa kijani kwa kupanda miti kando kando ya barabara na maeneo mengine. Amezitaka taasisi hizo kupanda miti mchanganyiko ikiwemo ya matunda.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu kwenye uzinduzi wa upandaji miti zaidi ya 1000 uliofanyika katika chanzo cha maji cha Miwaleni Kata ya Kahe Wilayani Moshi Aprili 25,2023 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo MIAKA 59 YA MUUNGANO, ”UMOJA NA MSHIKAMANO NDIYO NGUZO YA KUKUZA UCHUMI WETU.
Mhe. Babu ametoa wito kwa viongozi na watumishi wote wa Mkoa kuhakikisha kuwa miti iliyopandwa na itakayoendelea kupandwa inatunzwa na kuelekeza kila familia kupanda na kutunza angalau miti mitano (5) kila mwaka kulingana na ukubwa wa eneo ili kurejesha Kilimanjaro ya kijani kama ilivyokuwa hapo awali hii ni kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanyika katika Mkoa wetu jambo linalopelekea mabadiliko ya tabia nchi na kukauka kwa vyanzo vya maji, mvua kuchelewa kunyesha na wakati mwingine kunyesha mvua kidogo hali inayopelekea kuwa na uhaba wa chakula katika maeneo mengi ya Mkoa wetu na nchi yetu kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Babu amesema Muungano wetu umedumu kutokana na mizizi yake kujikita kwa wadau wakuu wa Muungano ambao ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, umakini na usikivu wa viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufuatilia kwa karibu changamoto zinazojitokeza na kuzipatia ufumbuzi umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha Muungano. Ameendelea kusema utamaduni uliowekwa na viongozi wetu wakuu wa nchi wa kuwa na vikao vya pamoja vya kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza kwa kuzingatia misingi ya umoja, haki, usawa na mshikamano, umeimarisha na kudumisha Muungano kwa kiasi kikubwa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilmanjaro Bw. Tixon Nzunda amesema katika kampeni hii ya kurudisha outo wa asili wa Mkoa wa Kilimanjaro utunzaji wa mazingira utaanzia kwenye ngazi ya Kaya, Kitongoji, Kijiji, Kata, Halmashauri na ngazi ya Mkoa.
Nzunda ameendelea kusema kunahaja ya kuwajengea wananchi uwezo na wadau wa ndani ya mkoa kuona umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa faida za vizazi vya sasa na vya baadaye, vile vile kujenga mwitikio kwa wadau kupenda, kuthamini, kupanda, kutunza na kuendeleza kazi ya utunzaji wa mazingira.
Akiwasilisha taarifa ya Wilaya Afisa Maliasili na Mazingira Wilaya ya Moshi Bw Inno Paul amesema takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha kuwa jumla ya miche ya miti 25,150 imepandwa katika msimu wa vuli kwa kushirikiana na wadau wa mazingira.
Bw.Paul amesema halmashauri imeanza kutekeleza mfumo wa Masijala ya Miti(Tree Registry System) ambapo katika mfumo huo miti yote itakayopandwa itasajiliwa kwa kuchukuliwa taarifa muhimu ambazo ni pamoja na namba ya mti, aina ya mti, data za majira ya nukta, mahali, na afya ya mti. Amesema faida ya mfumo huu ni kuchukua taarifa za maendeleo ya miti iliyopandwa mwaka hadi mwaka itasaidia kuongeza ufanisi wa miti iliyopandwa.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa