Mkoa wa Kilimanjaro umepewa heshima kubwa na Serikali ya Awamu sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024. Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 02 April, 2024 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi (MoCU) uliopo katika Manispaa ya Moshi. Aidha, baada ya uzinduzi huu Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri zote Saba (07) ndani ya Mkoa kuanzia tarehe 02/04/2024 hadi tarehe tarehe 08/04/2024.
Pamoja na ujumbe na maudhui muhimu ya mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024. Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu zinaenda sanjari na kumbukizi ya matukio adhimu katika Taifa letu ambayo ni;
Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuunda taifa la Tanzania,
Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo zilianza rasmi mwaka 1964, sambamba na;
Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 zinaadhimisha kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha muasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwaka huu ujumbe wa Mwenge wa Uhuru utahusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uhifadhi wa Mazingira chini ya Kaulimbiu isemayo, “Tunza mazingira na Shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu’’.
Aidha, pamoja na ujumbe huu mkuu zipo jumbe za kudumu ambazo zinawekewa mkazo kila mwaka na mwenge wa Uhuru kuhusu: -
•Mapambano dhidi VVU/UKIMWI, chini ya kauli mbiu isemayo; “Jamii iongoze kutokomeza UKIMWI”.
•Mapambano dhidi ya Malaria, chini ya kauli mbiu; “Ziro Malaria Inaanza na Mimi - Nachukua hatua kuitokomeza”.
•Mapambano dhidi ya dawa za kulevya, chini ya kauli mbiu isemayo; “Zingatia Utu; boresha huduma za Tiba na Kinga”.
•Mapambano dhidi ya rushwa, chini ya kauli mbiu isemayo; “Kuzuia Rushwa ni Jukumu lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu”.
•Uzingatiaji wa Lishe Bora, chini ya kauli mbiu isemayo; “Lishe sio kujaza Tumbo; Zingatia unachokula”.
Ratiba ya Mbio za Mwenge wa Uhuru ndani ya Mkoa;
Baada ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi, Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 zitafanyika Kimkoa kwa kila Halmashauri kwa ratiba ifuatayo:-
-Tarehe 02/04/2024 – Wilaya ya Moshi- Manispaa ya Moshi
-Tarehe 03/04/2024 – Utakuwa Wilaya ya Moshi - Halmashauri wa Moshi
-Tarehe 04/04/2024 – Utakuwa Wilaya ya Hai
-Tarehe 05/04/2024 – Utakuwa Wilaya ya Siha
-Tarehe 06/04/2024 – Utakuwa Wilaya ya Rombo
-Tarehe 07/04/2024 – Utakuwa Wilaya ya Mwanga
-Tarehe 08/04/2024 – Utakuwa Wilaya ya Same.
Baada ya uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru halmashauri ya Manispaa ya Moshi itakua ya kwanza kati ya halmshauri zote 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupokea na kukimbiza Mwenge wa uhuru tarehe 02/4/2024 hivyo wananchi wote wa Mji wa Moshi na Viunga vyake mnaombwa kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi pamoja na kwenye maeneo yote ya miradi itakayopitiwa na Mwenge pamoja na kushiriki katika mkesha wa Mwenge.
Aidha, Tarehe 09/04/2022 – Tutakabidhi Mwenge wa uhuru kwa wenzetu wa Mkoa wa Tanga katika Kijiji cha Bendera, Kata ya Bendera Wilayani Same kuanzia saa 12:00 asubuhi hivyo wananchi wa Wilaya ya Same tunahamashishwa kiujitokeza kwa wingi kukabidhi Mwenge wa Uhuru.
Kwa upande wa Vyombo vyote vya habari ikiwa televisheni, Redio, magazeti pamoja na mitandao ya kijamii tushirikiane kuhamasisha wananchi juu tukio hili kubwa katika Mkoa wetu,
Tunafahamu Serikali inatambua uwepo wa vipaji mbalimbali katika mkoa wetu hivyo tunawahamasisha kutumia fursa hii kuonyesha vipaji vyao na kuvitumia kuhamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki katika uzinduzi wa mwenge.
Hata hivyo kama tulivyosema tukio hili la kitaifa ni kubwa tunatarajia kupokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali katika nchi yetu hivyo ni wakati wetu mzuri wa kutumia fursa hii vizuri katika kuongeza pato letu huku tukiwahudumia wageni wetu kwa ukarimu, uaminifu na uchangamfu kama ilivyotabia wa Wanakilimanjaro.
Shime wamiliki na watoa huduma mbalimbali kama huduma za malazi na chakula, huduma usafiri n.k kujipanga vizuri kwa kuboresha huduma hizo.
Kama ilivyodesturi ya wanakilimanjaro juu ya suala zima la usafi na utunzaji wa mazingira nachukua fursa hii kuwakumbusha tuendelee kudumisha suala zima la usafi katika makazi yetu, maeneo ya biashara, mitaa na maeneo ya wazi ya kijamii. Aidha, mitaro na barabara zetu ziwe safi wakati wote na tuepuke utupaji wa taka ovyo. Hata hivyo kwakua ni msimu wa masika nawakumbusha kupanda miti katika maeneo yetu kuihudumia na kuitunza.
Sisi Mkoa wa Kilimanjaro tunasema Mwenge umerudi nyumbani ikiwa na maana kwamba mwaka 1964 Mwenge wa Uhuru ulipandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro hivyo tunaona fahari miaka 60 baadaye mwenge wa uhuru umerudi kuzinduliwa Mkoani Kilimanjaro ndoamana tunasema Mwenge wa Uhuru umerudi nyumbani.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa