Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg. Ismail Ussi, ametoa wito kwa vijana wa Wilaya ya Rombo na maeneo mengine nchini kuchangamkia mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotolewa na Serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmshauri kwa lengo kajiinua kiuchumi.
Ndg. Ussi ametoa wito huo leo Julai 2,2025 wakati alipotembelea na kukagua kikundi cha Vijana Mapambano Mafundi uliopo Tarafa ya Mkuu – Ushiri wanaojihusisha na utengenezaji wa samani mbalimbali kama vile meza, viti, makabati, fremu na madirisha.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi. Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Ni jukumu la vijana kuchangamkia fursa hizi kwa kuunda vikundi na kuandika miradi ya maana,” alisema Ndg. Ussi.
Akiwa katika eneo la mradi huo, amepongeza ubunifu wa vijana wa Mapambano Ufundi kwa kutumia mikopo hiyo kujiajiri na kuajiri wenzao kupitia utengenezaji wa bidhaa za mbao ambapo ni hatua ambayo inachangia kupunguza tatizo la ajira na kuongeza kipato kwa vijana wa eneo hilo.
Akisoma taarifa Mwenyekiti wa kikundi hicho Nicky Gabriel Mng’anya amesema kikundi kilianza rasmi mwaka 2024 kikiwa na vijana 5 na kupatiwa mkopo wa milioni 20 kwa ajili ya kuendeleza shughuli yao na kimefanikiwa kwa kupata kandarasi ndogo ndogo kutoka kwa wananchi.
Bw. Nicky ameishukuru Halmashauri kwa kuwapatia mkopo huo usio na riba, na kuahidi kuutumia vizuri kwa kuendeleza shughuli zao za uzalishaji mali, huku wakitoa wito kwa vijana wengine kujitokeza kuchangamkia fursa hizo badala ya kukaa bila kazi.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa