WANANCHI wa kijiji cha Lang'ata bora wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wameondokana na changamoto ya matumizi ya maji yasiyo safi na Salama baada ya serikali kutekeleza mradi wa kisima cha maji safi.
Wananchi hao walitoa kilio chao hicho leo wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika kijijini hapo kuzindua kisima hicho chenye urefu wa mita 152 kilichogharimu milioni 80.181.
Akizungumza mbele ya Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, mmoja wa wananchi hao, Happiness Mathayo alisema kuwa walikuwa wanalazimika kutumia maji yasiyo safi na salama ya Bwawani hali iliyokuwa ikipelekea kupata magonjwa ya mlipuko.
"Furaha yetu sisi wakinamama ni kupata maji haya safi na salama maana tumekuwa tukitumia maji yasiyo safi ya Bwawa ambapo samaki huvuliwa huko huko, punda hufia huko, watoto wanaoga huko huko bwanani na kujisaidia kwa hiyo sisi magonjwa ya mlipuko yalikuwa hayachezi mbali kila wakati tumekuwa watu wa kuharisha na kutapika" Alisema Happiness.
Alisema kuwa, kupitia mradi huo ambao umetekelezwa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuwatua wakinamama ndoo kichwani na kuwafanya kutowapeleka watoto zahanati kila mara kwa ajili ya magonjwa ya mlipuko.
Aliongeza kuwa, kwa mambo makubwa aliyofanya Rais ifikapo mwezi Oktoba watamlipa madeni yake kwa kumpa kura nyingi na za kishindo ili kumlipa kutokana na kazi kubwa alizozifanya.
Kwa upande, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismail Ali Ussi alisema kuwa, Mwenge huo umekuwa na lengo la kuleta matumaini pasipo na matumaini na wananchi walikuwa na tatizo la maji kwa muda mrefu lakini Serikali ya awamu ya sita imeweza kutatua kwa vitendo.
"Kwa mara ya kwanza Rais Dkt. Samia akiwahutubia wananchi kupitia ndani ya Bunge la Jamhuri moja ya jambo ambalo aliwaahidi Wananchi ni swala zima la kuhakikisha anaenda kutengeneza na kuboresha miundombinu ya maji safi na salama ndio maana leo kupitia Wizara ta maji imekuwa ikitatua kero za maji vijijini' alisema Ussi.
Kiongozi huyo, alisema kuwa eneo hilo lilikuwa linakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya maji safi na salama lakini Rais ameliona hilo na kwa upendo mkubwa kwa Wananchi Mwenge wa Uhuru umekuja kuweka amani, upendo na Heshima ambayo Dkt. Samia aliwaahidi wanalang'ata.
Aidha aliwataka Wananchi kuulinda na kuitunza miundombinu hiyo ya maji safi na salama ili iweze kudumu na kuwahudumia kwa muda mrefu kwani Serikali imetumia fedha nyingi.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa Mwenge, Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini wilaya ya Mwanga, Mhandisi Christine Kessy alisema kuwa, kisima cha Lang'ata Bora ni miongoni mwa programu ya visima 900 inayotekelezwa na Wizara ya maji.
Mhandisi Christine alisema kuwa, utekelezaji wa mradi ulianza Oktoba 2024 na kukamilika Februari 2025 ambapo walichimba kisima chenye urefu wa mita 152 ambacho kina uwezo wa kutoa maji lita 14000 kwa saa ambapo utawahudumia wananchi wapatao 3340.
Alisema kuwa, gharama za mradi huo ni shilingi milioni 80,181,620. kutoka benki ya Dunia kupitia programu ya PforR na kwa sasa umeshakamilika na kutoa maji kwa wananchi wa kijiji cha Lang'ata na Handeni.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa