Katika juhudi za kudhibiti na kutatua mgogoro wa muda mrefu wa ardhi baina ya Wakulima na Wafugaji katika kijiji cha Ruvu Marwa, wilayani Same, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ametoa siku 14 kwa wakulima na Wafugaji wa kijiji hicho wanaofanyakazi zao za kilimo na ufugaji katika eneo la ekari 2787 kupisha wataalamu kutoka ofisi za ardhi mkoa na wilaya kwa kushirikiana na pande zote mbili kupata suluhu ya matumizi bora ya ardhi.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho Agosti 20, 2025 Mhe. Babu alieleza kuwa mgogoro huo hauwezi kuachwa uendelee na kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila upendeleo.
"Katika eneo hili la hekari 2,787, Wafugaji wasiendelee kulitumia na Wakulima nao wasifanye shughuli yoyote hadi ndani ya siku 14 suluhu ipatikane. Tunahitaji suluhisho la pamoja, si mivutano ya kila mwaka," alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Akiwa ameambatana na viongozi wa wilaya, wataalamu wa ardhi na kilimo, Babu aliagiza shughuli zote zilizokuwa zikiendelea kwenye eneo hilo kusitishwa mara moja ili kutoa nafasi kwa majadiliano ya kina.
Katika hatua nyingine, aliahidi kupeleka wataalam kutoka ofisi yake kwenda kutathmini maeneo ya wakulima yanayoathiriwa na mafuriko kila mwaka, ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa na miundombinu ya kudhibiti maji kuingia mashambani.
Serikali imetoa wito kwa wakazi wa Ruvu Marwa Wakulima na Wafugaji kudumisha amani, mshikamano na utulivu bila kuangalia tofauti za kikabila, kidini wala maisha ya mtu.
"Ninyi ni Watanzania, rudisheni mahusiano yenu. Amani ndiyo msingi wa maendeleo. Hatutaki kila siku tuwe tunaleta polisi. Na kuhusu Mwenyekiti wa kijiji, hiyo ni kazi yangu na chama tutachukua hatua stahiki," aliongeza Babu.
Katika risala yao kwa Mkuu wa Mkoa, wakulima kupitia kwa msemaji wao Penueli Mkomwa, walieleza kuwa wamekuwa wakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara katika bonde la Ruvu, hali inayowasababishia hasara kubwa.
Mkomwa alieleza kuwa lipo eneo la wazi ambalo halijaathiriwa na mafuriko na linaweza kutumika kwa muda, lakini eneo hilo ni sehemu ya pori tengefu, hivyo kuhitaji uamuzi wa Serikali kuhusu matumizi yake
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa