WAFANYABISHARA Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kushirikiana kwa karibu na serikali katika kuboresha mazingira ya biashara ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote wa mkoa huo
Wito huo umetolewa Jana katika kongamano la wafanyabiashara ndogondogo lililofanyika katika soko la Mbuyuni, mjini Moshi likiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava alisema serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kutatua matatizo yanayowakumba wafanyabiashara wadogo, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa jamii.
"Serikali ni chombo chenu mnachotakiwa shirikiana nacho ili kutatua matatizo yanayowakabili , pia mikopo ipo kwenye halimashauri zetu mjinge kwenye vikundi mpate mikopo hiyo iwasaidie KATIKA kukuza biashara zenu,
Hii itawasaidia kutoka kwenye biashara ndogo ndogo kwenda kwenye biashara kubwa. muweze kulipa Kodi, kutoka ajira kwa vijana na kubadilisha mfumo wa maisha yetu na familia zetu,"alisema Mzava
Awali akimkaribisha mkuu huyo, katibu tawala ya Moshi, Shabani Mchomvu, alisema serikali imepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kwa kutumia mifumo ya kidijitali, ambayo imeongeza uwazi, usimamizi na urahisi wa huduma.
Alisema jumla ya wafanyabiashara 3,000 wamesajiliwa kupitia mfumo wa Wezesha Portal, kati yao wanaume ni 1,070 na wanawake 1,930, ikiwa ni hatua muhimu katika kutambua na kurasimisha biashara ndogondogo.
"Zaidi ya milioni 317 zimetolewa kama mikopo kwa wafanyabiashara 145 kupitia Benki ya NMB, fedha ambazo zimeelekezwa kwenye kukuza mitaji na upanuzi wa biashara. Mikopo hiyo isiyo na riba imekuwa chachu ya mabadiliko kwa wengi, hasa wanawake na vijana waliokuwa na tatizo ya mitaji"
Alisema pia Serikali pia imefanikiwa kujenga, kukarabati na kurasimisha maeneo 41 ya biashara katika wilaya mbalimbali za mkoa, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa maeneo rasmi ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogowadogo.
Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Juliana Mtolela, alisema kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuwezesha makundi maalum kwa kuwapatia mitaji, mafunzo na fursa za kiuchumi.
“Kupitia programu na mikakati mbalimbali ya kitaifa, serikali imefanikiwa kuwafikia maelfu ya wafanyabiashara wadogo nchini kwa kuwapatia mitaji, mafunzo ya ujasiriamali, pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha,” alisema Mtolela,
Wafanyabiashara walioshiriki kongamano hilo walieleza kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali, huku wakisisitiza umuhimu wa kupatiwa elimu ya masoko na usimamizi wa fedha ili kuongeza ufanisi katika biashara zao.
Baadhi ya wafanyabiashara waliopatiwa mikopo walieleza kuwa mitaji hiyo imewasaidia kuongeza bidhaa, kuboresha huduma na kuongeza ajira kwa vijana wa maeneo yao. Walisema mafanikio hayo yameanza kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha yao na ya jamii inayowazunguka.
Viongozi wa vikundi vya wafanyabiashara walipongeza serikali kwa kujenga miundombinu rafiki ya biashara kama vile vibanda vya kisasa, mabanda ya masoko na miundombinu ya maji na umeme, ambayo imeboresha mazingira ya kazi na kuvutia wateja zaidi.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta binafsi kuhakikisha kuwa biashara ndogondogo zinakua na kuwa endelevu, huku ikiwahimiza wafanyabiashara kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa ili kuimarisha mitaji yao.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa