Wananchi wa maeneo ya Kileo wilayani Mwanga na Hedaru wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, wameanza kunufaika na maboresho makubwa ya miundombinu ya barabara na daraja, yanayotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo kwa kuwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaolenga kuboresha maisha ya watu na kuzuia madhara yanayosababishwa na mvua za mara kwa mara.
Akizungumza Agosti 7, 2025, katika ziara yake ya siku moja eneo la Kileo, Babu alisema serikali inatekeleza ujenzi wa boxcalvert saba pamoja na kunyanyua tuta la barabara kufikia urefu wa mita 1.5, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutatua kero za muda mrefu za usafiri nyakati za mvua.
"Kileo ilikuwa korofi sana hasa wakati wa mvua. Serikali kupitia TANROADS imejenga boxcalvati 7 na mradi huu umefikia asilimia 31 ya utekelezaji. Tunatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 6 kukamilisha kazi hii," alisema Babu.
Akiwa katika eneo la Hedaru wilayani Same, RC Babu alitembelea ujenzi wa daraja jipya litakalogharimu shilingi bilioni 1.5, likilenga kuzuia madhara ya maji yanayotiririka kutoka milimani, ambayo yamesababisha athari kubwa kwa wananchi.
"Katika mvua za El Niño 2023/2024 tulipata adha kubwa sana. Wapo wananchi waliopoteza maisha. Mheshimiwa Rais ametoa fedha ili kukamilisha daraja hili kwa haraka. Tayari kazi imefikia asilimia 50 na tunatarajia kukamilika ifikapo Septemba 4 mwaka huu," aliongeza.
Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa mafanikio haya ni ya wananchi wote na akawataka kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
"Tuwe maaskari wa miundombinu yetu. Tukubali kubadilika na kuitunza kwa sababu changamoto zilikuwa zikitutesa kwa muda mrefu," alisema.
Akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa, Meneja wa TANROADS mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, alisema mkoa umepokea ufadhili wa shilingi bilioni 16.2 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja, njia za maingiliano, na usimamizi wa miradi mbalimbali ya barabara.
Ameeleza kuwa fedha hizo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhakikisha maeneo hatarishi yanapata ufumbuzi wa kudumu kupitia miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji.
Naye Msimamizi wa Mradi wa Kileo kutoka kampuni ya King Builders, Mhandisi Paul Mwanawima, alisema mradi unaendelea vizuri licha ya changamoto ya maji mengi kwenye eneo hilo.
"Maji yalikuwa mengi sana wakati tunaanza kazi, hali iliyoathiri hata mashine zetu. Lakini tumekabiliana na hali hiyo na tunaendelea vizuri. Tunatarajia kukamilisha kazi mwanzoni mwa Septemba," alisema Mhandisi Mwanawima.
Wananchi wa maeneo husika wameanza kuona manufaa ya miradi hiyo huku wengi wakisema kuwa usafiri umeimarika na wana imani kuwa baada ya kukamilika, matatizo ya mafuriko na mazao kuozea barabarani yatabaki kuwa historia.
Kwa ujumla, maboresho ya miundombinu katika mkoa wa Kilimanjaro yanaendelea kuwa chachu ya maendeleo na kiashiria cha dhamira ya dhati ya serikali kuboresha maisha ya wananchi kwa vitendo.
Mwisho
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa