Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa viashiria vyote 14 vya afua za lishe kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye Mfumo Jumuishi wa Lishe.
Mafanikio hayo yametajwa kuwa matokeo ya mshikamano mzuri kati ya viongozi wa wilaya, wakurugenzi na wadau wa maendeleo.
Akizungumza Agosti 12, 2025, katika kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe kilichofanyika ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, alisema hali ya utoaji wa fedha kwa mwaka huu wa fedha ni ya kuridhisha ukilinganisha na mwaka uliopita.
Hata hivyo, alisisitiza haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia lengo la asilimia 100 ya mafanikio.
“Sitaki kusikia suala la udumavu linaendelea mkoani. Watoto waliodumaa ni mzigo kwa familia na taifa. Lazima tutokomeze tatizo hili,” alisema Babu, akiwataka viongozi wote wa ngazi za wilaya, kata na vijiji kuipa lishe kipaumbele katika vikao na maadhimisho mbalimbali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa, alisema licha ya jitihada kubwa za serikali na wadau, bado changamoto za lishe duni, udumavu na utapiamlo zinaonekana katika baadhi ya halmashauri. Alibainisha kuwa tatizo hilo linahitaji uhamasishaji wa jamii kwa nguvu mpya.
Ofisa Lishe wa Mkoa wa Kilimanjaro, Rehema Napegwa, alieleza kuwa kiwango cha udumavu kiko kwenye asilimia 20, sawa na watoto takribani 40,000. Alionya kuwa mtoto akifikia miaka miwili akiwa amedumaa, uwezo wa kutibu hali hiyo huwa mdogo, jambo linaloathiri maendeleo ya kiafya na kiakili kwa muda mrefu.
Rehema alisema moja ya changamoto kubwa ni muamko mdogo wa wanaume kushiriki katika masuala ya lishe vijijini, jambo linalochangia kuendeleza tatizo la udumavu.
“Wanaume ndio watoa maamuzi ya mwisho kuhusu chakula cha familia. Bila wao kushiriki kwenye elimu ya lishe, maamuzi mengi hubaki duni,” alisema.
Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wa ngazi za kijiji na kata hawajaonyesha utayari wa kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika mafunzo na mikutano ya afya na lishe.
“Wakati wa maadhimisho, elimu mbalimbali hutolewa ikiwemo jiko darasa na mbinu za kuinua kipato. Lakini bila wanaume, matokeo hayawi ya kuridhisha,” alifafanua.
Akitoa takwimu, Rehema alisema asilimia 56 ya watoto hupewa vinywaji vyenye sukari kama juisi na soda, hali inayoweza kusababisha uzito kupita kiasi na kuathiri ukuaji wa ubongo. Alipinga dhana potofu kuwa mtoto mnene ana afya bora, akisema lishe bora si suala la wingi wa chakula pekee bali ubora wake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala, alisema wilaya hiyo imejipanga kutoa zaidi ya shilingi elfu tatu kwa kila mtoto kwa mwaka huu wa fedha — kiwango kilicho juu ya kiwango cha kitaifa cha shilingi elfu moja. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila mtoto anapata mlo kamili.
Mangwala alisema sasa ajenda ya lishe imewekwa kama kipengele cha kudumu katika mikutano yote ya wilaya na vijiji. “Nawaomba wanaume wajitokeze na kuwekeza kwenye lishe ya wanawake wajawazito na watoto. Hii ndiyo njia ya kupata kizazi chenye afya na akili timamu,” alisema.
Aliongeza kuwa watoto bora wa leo ndio viongozi bora wa kesho, hivyo uwekezaji kwenye lishe ni uwekezaji wa moja kwa moja kwenye maendeleo ya taifa.
Mkataba wa lishe ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kutokomeza utapiamlo na kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira yenye tija kimwili, kiakili na hata kiroho, lengo likiwa kujenga taifa lenye nguvu kazi bora na mustakabali imara wa maendeleo.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa