Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Dkt. Anna Mghwira amewataka wataalam wa wakala wa barabara nchini TANROADs pamoja na wa mamlaka ya barabara vijijini TARURA wanaojenga madaraja yaliyoharibika kutokana na mvua za vuli wilayani handeni mkoani Tanga kuwa wazalendo na kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo katika kiwango kinachokubalika ili iweze kuwasaidia wananchi katika vipindi vyote vya mwaka.
Dkt. Mghwira ameyasema hayo baada ya kukagua madaraja matatu yanayojengwa upya wilayani Handeni ambayo yalikaktika kabisa baada ya kuzidiwa nguvu na maji ya mvua katika mito.
Katika ziara hiyo Dkt. Mghwira amepata fursa ya kuona uharibifu mkubwa wa mabwawa ya kuhifadhia maji yaliyokuwa yakitumiwa na wanachi wa wilaya Handeni kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani.
Aidha Dkt. Mghwira amewashauri wataalam wa mabwawa ya kuhifadhia maji wajikite zaidi katika kutafiti namna ya kujenga mabwawa madhubuti yatakayoweza kuhilimili misukosuko endapo kutatokea majanga yakiwemo mafuriko.
Dkt. Mghwira aliyeambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro pamoja na baadhi ya wataalam alifanya ziara ya siku moja mkoani Tanga tarehe 3/11/2017 ili kujionea hali ya uharibifu wa miundombinu uliyoikumba mkoa huo pamoja na kutoa pole kwa viongozi na wananchi wa mkoa wa Tanga kutokana na vifo vya baadhi ya wananchi vilivyotokana na mvua za vuli.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela amemshukuru Dkt. Mghwira kwa moyo wake wa utu uliomsukuma kutenga muda wake ili kutoa pole kwa watu wa Tanga.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa