Katika kipindi cha miaka miwili kuanzia tarehe 19 Machi, 2021 hadi 19 Machi, 2023 Mkoa wa Kilimanjaro umepokea jumla ya shilingi bilioni 620.224 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 717 katika sekta za Afya, Elimu, Miundombinu ya barabara, Maji, Kilimo na Mifugo, Usafirishaji na Uchukuzi, Mipango Miji na Uwezeshaji wa kiuchumi wananchi. Fedha zilizotolewa zimeuwezesha mkoa kufanya mambo muhimu yafuatayo:-
SEKTA YA AFYA
Katika kipindi cha miaka miwili, Mkoa kwa sekta ya afya pekee umepokea na kutekeleza jumla ya miradi 116 yenye thamani ya shilingi bilioni 45.0 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Baadhi ya miradi hiyo ni kama ifuatavyo: -
Ujenzi wa jengo la mionzi (bunker) idara ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC – Mradi umepokea shilingi bilioni 3 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma ya matibabu ya saratani na kupunguza adha ya wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kufuata huduma ya matibabu hospital ya Ocean Road – Dar es Salaam na nje ya nchi.
Ukarabati wa jengo la kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC – Mradi huu umepokea shilingi milioni 499 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kutoa huduma kabambe kwa wagonjwa mahututi wafikao katika hospital.
Ujenzi wa Maabara ya kisasa ya Afya ya Jamii ya Usalama wa Kibaiolojia ngazi ya tatu katika hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (Kibong’oto Public Health Biosafety Laboratory Level III) -Mradi umepokea Shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ujenzi wa jengo shilingi bilioni 12.5 na vifaa shilingi bilioni 10. Maabara itasaidia katika ufuatiliaji na uchunguzi wa magonjwa ya kuambukiza kwa kanda ya Kaskazini na taifa kwa ujumla kupitia tafiti za kitaifa na kimataifa.
Ukarabati wa jengo la Wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto – Mradi umepokea shilingi bilioni1.9 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa jengo la wagonjwa mahututi, baada ya ukarabati kukamilika, jengo linalaza wagonjwa mahututi 20 kwa siku kutoka watu 3 - 5 wa awali.
Ujenzi wa Jengo la Ghorofa katika Hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto – Mradi umepokea shilingi milioni 687 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mionzi (radiologia) kwa lengo la kutoa huduma za kiuchunguzi za mionzi (X-ray), CT scan, MRI, fluoroscopy, mamograph na ultrasound.
Ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi - Mradi umepokea shilingi bilioni 5.5 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kutoa huduma kambambe za afya ya uzazi kwa mama, baba na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kuondokana na rufaa za kwenda katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya KCMC na Hospitali nyingine.
Ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo mashine ya CT - Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi – Mradi umepokea Shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya ununuzu wa vifaa tiba kama CT-Scan, digital x- ray, ultrasound kuwekwa katika jengo la mama na mtoto, jengo la dharura (EMD) na ICU. Lengo likiwa ni kuimarisha huduma za kiuchunguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuondokana na rufaa kwa wagonjwa.
Ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi – Mradi umepokea Shilingi milioni 149 kutoka serikali kuu kwa ajili ya uimarisha huduma za wagonjwa mahutihuti na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali ya kanda ya KCMC.
Ujenzi wa Jengo la Dharura (EMD) Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi – Mradi umepokea shilingi milioni 756 kutoka serikali kuu kwa ajili ya kuanzisha huduma za dharura katika hospitali ya rufaa ya mkoa. Huduma hizi zinasaidia sana kutoa huduma kwa haraka kwa wagonjwa na kuepusha vifo visivyo vya lazima. Jengo limekamilika na huduma zimeanza kutolewa kwa wagonjwa.
Ujenzi na ukamilishaji wa Hospital za Halmashauri – Mkoa umepokea shilingi bilioni 8.9 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya 4 katika halmashauri za Manispaa ya Moshi, Same DC, Mwanga DC na Moshi DC. Aidha, fedha hizo zimetumika kukamilisha majengo yaliyoanza kujengwa katika hospitali za halmashauri za Siha DC, Hai DC na Rombo DC. Miradi hiyo ni utekelezaji wa será ya afya ya kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na hospital yake kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma za afya karibu na maeneo yao.
Ujenzi na Ukarabati wa vituo vya afya. - Mkoa umepokea shilingi bilioni 8.6 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya 22 katika halmashauri za Same vituo 5, Mwanga vituo 4, Rombo vituo 2, Moshi DC vituo 3, Hai vituo 4, Siha vituo 2 na Moshi Manispaa vituo 2. Miradi inayotekelezwa katika vituo hivyo ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), Maabara, Upasuaji, Jengo la Wazazi, Jengo la mionzi, Wodi za kulaza wagonjwa, Kichomea taka, jengo la kliniki ya mama na mtoto, jengo la kufulia, Ujenzi wa shimo la kutupia kondo la nyuma (Placenta pit) na Njia za kupitia wagonjwa (walk ways)
Ujenzi na ukamilishaji wa zahanati – Mkoa umepokea shilingi bilioni 2.4 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya na ukamilishaji wa maboma ya zahanati. Fedha zilizopokelewa zimejenga na kukarabati zahanati 48 Katika halmashauri za Same zahanati 14, Mwanga zahanati 7, Rombo zahanati 5, Moshi DC zahanati 10, Hai zahanati 7 na Siha zahanati 5. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia fedha hizo kwani zimefanikisha kukamilisha miradi iliyoanzishwa kwa juhudi za wananchi.
SEKTA YA ELIMU
Katika sekta ya elimu, Mkoa umepokea shilingi bilioni 17.21 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, maabara za masomo ya sayansi na kompyuta na ujenzi wa majengo ya utawala katika shule. Utekelezaji wa miradi hii umesaidia sana kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa darasa la nne, saba, kidato cha pili, cha nne na cha sita.
Ujenzi wa Shule Mpya za Kata za Sekondari
Kiasi cha shilingi bilioni 4.2 kilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya tisa za Kata za sekondari katika Halmashuari za Hai Dc shule 1, Moshi DC shule 2, Moshi Manispaa shule 1, Mwanga DC shule 1, Rombo DC shule 1, Same DC shule 2 na Siha DC shule 1.
Ujenzi wa madarasa katika shule za sekondari
Katika kipindi cha miaka miwili mkoa umepokea shilingi Bilioni 8.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 401 katika shule za sekondari. Lengo la ujenzi wa madarasa haya ni kuziongezea madarasa shule zilizokuwa na upungufu mkubwa wa madarasa. Madarasa yamejengwa kwa mchanganuo ufuatao; - Hai DC madarasa 53, Moshi DC madarasa 115, Moshi Manispaa madarasa 32, Mwanga DC madarasa 19, Rombo DC madarasa 52, Same DC madarasa 88 na Siha DC madarasa 42. Ujenzi huu umesaidia sana wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wameweza kuanza masomo kwa asimilia 100 kwa idadi ya waliochaguliwa.
Ukarabati na Ujenzi wa madarasa ya Shule za Msingi na Shikizi
Ndani ya kipindi cha miaka miwili zimepokelewa shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya 134 katika shule za msingi kwa mchanganuo ufuatao; Same madarasa 5, Mwanga madarasa 22, Rombo madarasa 18, Moshi DC madarasa 38, Moshi MC madarasa 12, Hai DC madarasa 34 na Siha DC madarasa 5 na shule Shikizi madarasa 20 kwenye hlmashauri ya Mwanga madarasa 2, Rombo madarasa 2, Same madarasa 2 na Siha madarasa 14. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 831 kimetumika kukarabati madarasa 138 ya shule za msingi.
Ujenzi wa matundu ya Vyoo
Katika kuboresha mazingira ya usafi na afya za wanafunzi mkoa ulipokea shilingi milioni 455.5 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 414 yaliyojengwa katika shule za msingi zilizopo kwenye halmashauri za Mwanga matundu 60, Rombo matundu 47, Moshi DC matundu 88, Moshi MC matundu 137, Hai DC matundu 34 na Siha DC matundu 48.
Magari ya Idara ya elimu Sekondari
Katika kuboresha usimamizi wa ubora wa elimu, Mkoa umepokea magari mawili kwa ajili ya idara elimu sekondari kwa halmashauri za Wilaya ya Same na Mwanga. Tunaishukuru serikali kwani magari haya yanasidia sana katika shughuli za ufuatiliaji na usimamizi
Mgao wa Vishikwambi kwa Waalimu
Kupitia zoezi la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, mkoa umepokea vishikwambi 11,813 kwa ajili ya waalimu wote wa shule za msingi na sekondari wa mkoa wa Kilimanjaro. Tunaishukuru serikali kwa msaada mkubwa kwa waalimu kwani vishikwambi hivi vimewezesha waalimu kuongeza ujuzi na maarifa kwa njia ya elimu mtandao, kuhifadhi taarifa na kumbukumbu muhimu za kitaaluma na kiutawala hivyo kuboresha uandaaji na ufundishaji mashuleni.
SEKTA YA NISHATI
Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya sita hadi sasa, Mkoa kupitia Sekta ya Nishati umepokea shilingi bilioni 21.59 kwa ajili ya kuboresha, kuunganisha na kutekeleza miradi mipya ya umeme ndani ya mkoa. Usambazaji wa umeme kupitia shirika la TANESCO umefikia asilimia 100 mijini, vijijini kupitia REA umefikia 97.9% sawa na vijiji 508 kati ya 519 vilivyounganishiwa huduma ya umeme na vitongoji 1,911 sawa na asilimia 84.6 kati ya 2,260 vimeunganishwa na huduma. Aidha, jumla ya wateja 68,300 wameunganishiwa umeme katika mkoa mzima.
4.SEKTA YA MAJI
Mkoa kupitia Mamlaka za Maji umepokea shilingi bilioni 358.43 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji ndani ya mkoa. Jumla ya Miradi 50 inatekelezwa kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini (MUWSA), Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) na Wizara ya Maji. Katika kipindi cha miaka miwili miradi ifuatayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa kama ifuatavyo:-
Miradi inayotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)
NaHalmashauriIdadi ya MiradiGharama za ujenziHali ya utekelezaji
1Same DC10Bilioni 3.81
Miradi 7 kati 10 imekamilika
2Hai DC8Bilioni 3.33Miradi yote imekamilika
4Moshi DC6Bilioni 1.86Miradi 4 kati 6 imekamilika
5Mwanga DC6Bilioni 1.59
Miradi 3 kati 6 imekamilika
6Siha DC5Bilioni 1.80
Miradi yote imekamilika
7Rombo DC6Bilioni 2.34
Miradi 4 kati 6 imekamilika
JUMLA41
Bilioni 14.73
Miradi Inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini (MUWSA)
NaMradiGharama za MradiHali ya utekelezaji
1Mradi wa majisafi kata ya Old Moshi MasharikiMilioni 438Mradi huu umefikia asilimia 59 ambapo jumla ya bomba zenye urefu wa kilomenta 23 kati 39 zimekamilika
2Mradi wa majisafi kata ya MbokomuMilioni 226 Mradi huu umefikia asilimia 47 ambapo jumla ya bomba zenye urefu wa kilomenta 11.6 kati 24.7 zimekamilika
3Mradi wa majisafi kata ya Mwika kusiniMilioni 304 Mradi huu umefikia asilimia 67.1 ambapo jumla ya bomba zenye urefu wa kilomenta 22.9 kati 33.9 zimekamilika
4Mradi wa kata ya Uru Mashariki (Mnini)Milioni 167 Jumla ya mtandao wa mabomba ni kilometa 15. kazi katika eneo hili zimekamilika kwa asilimia 82
5Mradi wa majisafi kata ya MadoginiMilioni 500 Mradi huu umefikia asilimia 62.5 ambapo jumla ya bomba zenye urefu wa kilomenta 28.15 kati 94.8 zimekamilika
6Mradi wa majisafi kata ya kimochiMilioni 500 Mradi huu umefikia asilimia 58 ambapo jumla ya bomba zenye urefu wa kilomenta 20.30 kati 44.3 zimekamilika
7Mradi wa majisafi kata ya Marangu MasharikiMilioni 120 Mradi huu umefikia asilimia 31.7 ambapo jumla ya bomba zenye urefu wa kilomenta 5.9 kati 18.8 zimekamilika
8Mradi wa majisafi kata ya Njia PandaBilioni 2.4Mradi huu wenye jumla ya kilometa 14 umekamilika kwa asilimia 100
JUMLABilioni 4.66
Mradi wa maji Same – Mwanga – Korogwe
Mradi wa maji Same – Mwanga – Korogwe umetengewa shilingi Bilioni 339.026 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuendeleza mradi. Mradi huu ulikuwa umesimama kwa kipindi kirefu kutokana na ukosefu wa fedha.Tunamshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuupatia tena fedha za utekelezaji na kuruhusu kuhuishwa kwa utekelezaji wa mradi tarehe 13 Machi, 2023 uliowekwa saini na Mhe. Waziri wa Maji na kampuni ya Kharaf and Sons Ltd ya Nchini Kuwait ambayo ndio watekelezaji wa ujenzi wa mradi katika eneo la chanzo. Mradi utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha wastani wa lita 103,650 kwa siku na wananchi wapatao 438,820 watakuwa wananufaika na mradi huo kutoka kwenye maeneo ya Mwanga, Same na Korogwe.
UCHUMI NA UZALISHAJI (KILIMO, MIFUGO, UTALII, MAZINGIRA NA MISITU
Katika kipindi cha miaka miwili chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mkoa umeweza kuweka nguvu kubwa katika kuboresha shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kujenga mazingira bora ya utalii na uhifadhi wa mazingira. Baadhi ya mambo yaliyofanyika katika kipindi cha miaka miwili ni pamoja na;
Mbolea ya Ruzuku kwa Wakulima
Katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, Mkoa umepokea mbolea ya ruzuku tani 13,173.65 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.47 inayotarajiwa kutolewa kwa wakulima 251,317 kwa mchanguo ufuatao; Hai DC wakulima 37,686, Moshi DC wakulima 50,000, Moshi MC wakulima 2,513, Mwanga DC wakulima 17,124, Rombo DC wakulima 51,468, Same DC wakulima 67,256 na Siha DC wakulima 25,000. Kutokana na mbolea hiyo, mkoa unatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 1,426,635.27 za mazao ukilinganisha na tani 1,118,144 za mwaka 2020/2021 kipindi ambacho ruzuku haikutolewa.
Ujenzi wa Skimu za Umwagiliaji
Kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya nafaka na mbogamboga, Mkoa umepokea Shilingi bilioni 1.47 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miradi miwili ya umwagiliaji katika halmashauri ya Wilaya ya Siha, Mradi wa Bwawa la Orumwi wenye thamani ya Shilingi 410,287,806 na halmashauri ya Wilaya ya Mwanga , Mradi wa Skimu ya umwagiliaji Kirya wenye thamani ya Shilingi 1,064,674,871.20. Kupitia miradi hiyo halmashauri zinatarajia kuongeza uzalishaji Mpunga kutoka tani 270 hadi tani 540, Mahindi kutoka tani 900 hadi tani 1,260, Mbogamboga kutoka tani 2000 hadi 4000, Kahawa kutoka tani 0.5 kwa hekta hadi tani 0.7 na Ndizi kutoka tani 3.5 kwa hekta hadi tani 5.
Ugawaji wa pikipiki kwa Maafisa Ugani
Ili kuongeza uwajibikaji kwa maafisa ugani, Mkoa umepokea pikipiki 245 zenye thamani ya Shilingi milioni 735 kwa ajili ya maafisa ugani kutoka kutoka halmshauri zote za mkoa wa Kilimanjaro. Mgawanyo wa pikipiki kwa kila halmashauri ni kama ifuatavyo;- Siha DC pikipiki 23, Mwanga DC pikipiki 37, Rombo DC pikipiki 29, Hai DC pikipiki 39,Same DC pikipiki 44, Moshi DC pikipiki 60, na Moshi MC pikipiki 12, sekretarieti ya mkoa pikipiki 1.
Ujenzi wa majosho na ugawaji wa madawa ya kuogesha mifugo
Katika kuhakikisha magonjwa ya mifugo yanadhibitiwa, Mkoa umepokea Shilingi milioni 229.97 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 9 katika halmashauri za Siha majosho 2, Hai josho 1, Mwanga majosho 2 , Same majosho 3 na Moshi josho 1. Dawa za kuogesha mifugo lita 1,066 zimenunuliwa. Kutokana na matumizi ya dawa hizo mkoa umeweza kupunguza vifo vya mifugo dhidi ya magonjwa yanayoenezwa na kupe kwa asilimia 12.
Ujenzi wa kituo cha kukusanyia maziwa Wilaya ya Hai
Mkoa umepokea shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kukusanya na kupooza maziwa katika kata ya Masama Wilaya ya Hai. Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia wafugaji wapatao 300 kupata soko la uhakika la maziwa na jumla ya lita 1,500 zitakusanywa na kupoozwa katika kituo husika kwa siku.
Uboreshwaji wa miundombinu ya Utalii
Mkoa umepokea Shilingi bilioni 4.62 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya utalii katika maeneo ya Hifadhi za Taifa za Mlima Kilimanjaro, Mkomazi na Msitu wa Chome kupitia fedha za UVIKO 19. Matokeo ya maboresho ya miundombinu na filamu maarufu duniani ya ‘’The Royal Tour’’ idadi ya watalii wanaotembelea mkoa kupitia uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) imeongezeka kutoka watalii 46,199 mwaka 2020 hadi kufikia watalii takribani 61,801 mwaka 2022. Ongezeko hili limechangia kuongezeka kwa ajira, mzunguko mkubwa wa biashara na hatimaye kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Uboreshaji wa Mazingira
Kwa kuzingatia msisitizo wa utunzaji wa mazingira unaotolewa na Serikali ya awamu ya sita, Mkoa umeweza kuratibu zoezi la upandaji wa miti kutoka miti 7,413,160 hadi kufikia miti 8,709,200. Mkoa unaendelea kusimamia ustawi wa miti yote iliyooteshwa, kuzuia ukataji miti hovyo na uhamasiishaji wa upandaji wa miti katika halmashauri zote.
SHUGHULI ZA UWEKEZAJI
Kutokana na mazingira mazuri na Sera nzuri za uwekezaji nchini, kwa kipindi cha miaka miwili Mkoa umeweza kuvutia wawekezaji waliowekaza katika viwanda, mashamba ya kuku na utalii yenye thamani ya shilingi bilioni 43.1. Uwekezaji huu umefanyika katika halmashauri ya Wilaya ya Siha mradi wa shamba kubwa la kuku bibi (Grandparent stock) lenye thamni ya shilingi bilioni 36 na shamba la wanyama pori Serval Wildlife lenye thamani ya Shilingi bilioni 4.6 na katika halmshauri ya Wilaya ya Same mradi wa Mamba Myamba Ginger Growers Company Limited wenye thamani ya shilingi Bilioni 2.5.
HALI YA UKUSANYAJI WA MAPATO NA UWEZESHWAJI WA WANANCHI KIUCHUMI
Ukusanyaji wa Mapato
Kutokana na maboresho ya sera za ukusanyaji wa mapato nchini na mazingira mazuri na rafiki yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita kwa wafanya biashara, Mkoa umeweza kukusanya shilingi Bilioni 468.944 sawa na asilimia102.6 kati ya lengo la kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 457.08 kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Aidha, Mapato ya ndani ya halmashauri yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 23.873 hadi bilioni 24.512 sawa na asilimia 103.
Mikopo ya asilimia 10 kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu - Shilingi bilioni 4.216
Kupitia asilimia 10 ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Mkoa umetoa shilingi Bilioni 4.216 kwa kipindi cha miaka miwili. Mikopo imeweza kutolewa kwa vikundi vya Wanawake 420, Vijana 182 na watu wenye ulemavu vikundi 187. Wanavikundi wameweza kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ya kilimo, ufugaji, karakana za uchomeleaji, mashine za kusaga na ujasiriamali ambazo zinawasaidia kuendesha maisha yao.
Mpango wa kunusuru kaya zenye Kipato cha chini (TASAF)
Mkoa umetoa shilingi bilioni 9.67 kupitia mpango wa kunusuru kaya zenye kipato cha chini (TASAF) Awamu ya tatu ambapo jumla ya kaya 41,709 kutoka katika vijiji 519 na Mitaa 60 zimeweza kunufaika. Kiasi cha fedha kilichotolewa ni mara mbili ya kiasi cha fedha kilichotolewa wakati wa serikali ya awamu iliyopita.
SHUGHULI ZA UTAWALA BORA
Katika kuimarisha masuala ya utawala bora, Mkoa umepokea shilingi bilioni 3.97 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Utawala katika Halmashauri za Wilaya ya Moshi na Mwanga.
Aidha, Shilingi bilioni 1.84 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Maafisa Tarafa 22 katika Wilaya zote za mkoa wa Kilimanjaro. Lengo la ujenzi wa ofisi hizo ni kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa maafisa tarafa na halmashauri katika kuwahudumia wananchi.
Anuani za Makazi na Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022
Ili kuweka sawa mipango ya serikali na wananchi kwa ujumla, Mkoa uliendesha zoezi la Anuani za makazi. Jumla ya Anuani 421,970 ziliweza kusajiliwa katika mkoa wa Kilimanjaro sawa na asilimia 100.45. Aidha, jumla ya wananchi 1,861,934 ikiwa wanawake 954,298 na wanaume 907,636 waliweza kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
SEKTA YA ARDHI
Utatuzi wa mgogoro wa ardhi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa furaha, amani na kutekeleza shughuli zao za kiuchumi, Serikali ya Awamu ya sita imefanya kazi kubwa sana ya kutatua migogoro ya ardhi baina ya wananchi kwa wananchi na wananchi na taasisi mbalimbali. Napenda mfahamu kwamba, Mkoa wetu umekuwa na mgogoro wa muda mrefu baina ya wananchi wa vijiji vinne (4) vya Sanya Station, Tindigani, Chemka na Mtakuja vilivyopo katika wilaya ya Hai na Kiwanja cha ndege cha KIA. Wananchi hao waliingia na kuishi ndani eneo linalomilikiwa na uwanja bila utaratibu.
Tunapenda kumshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upendo wake kwa wananchi kwa kuushughulikia na kuumaliza mgogoro huu katika kipindi cha muda mfupi baada ya kuridhia kufanyika kwa uthamini wa maeneo wanayoishi wananchi hao pamoja na wale wa vijiji vya jirani vya Mkoa wa Arusha. Kufuatia tathmini hiyo serikali itatoa jumla ya shilingi Bilioni 11.3 ambapo shilingi Bilioni 7.3 zitalipwa kwa wananchi wa wilaya ya Hai na shilingi Bilioni 4.04 zitalipwa kwa wananchi wa Wilaya ya Arumeru.
MIRADI ILIYOTEKELEZWA NA TARURA
Ujenzi wa barabara za lami
NaHalmashauriBarabaraUrefu Gharama za ujenziHali ya utekelezaji
1Hai DCSt Dorcus na TTCL9.4 KMBilioni 2.162Zimekamilika
2Moshi MCLema, Msitu, Kilimanjaro, Sekue Toure na Kambaita7.1 KMBilioni 1.646Zimekamilika
3Mwanga DCMsuya0.86 KMMilioni 381.917Imekamilika
4Rombo DCStand0.65 KMMilioni 926.733Imekamilika
5Siha DCDC- Karansi – Makiwaru, Sanya Juu – Naibili - KIA4.6 KMBilioni 1.067Ujenzi unaendelea
JUMLA18.0146 KMBilioni 6.183
Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe na madaraja
NaHalmashauriUrefu Gharama za ujenziHali ya utekelezaji
1Hai DC26.1KMBilioni 2.08Kazi zinaendelea
2Moshi DC523.01KMBilioni 3.6Kazi zinaendelea
3Moshi MC40.17KMBilioni 2.8Kazi zinaendelea
4Mwanga DC502.65 KMBilioni 3.8Kazi zinaendelea
5Rombo DC116.53 KMBilioni 2.6Kazi zinaendelea
6Same DC180.23 KMBilioni 6.9Kazi zinaendelea
7Siha DC199.31 KMBilioni 1.07Kazi zinaendelea
JUMLA1,588 KMBilioni 22.85
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa