MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO ATOA SIKU 14 KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA SHULE YA SEKONDARI MKAMALA WILAYANI HAI
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ametoa siku 14 kwa mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkamala iliyopo Wilayani Hai kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ifikapo Mei 15, 2025.
Mhe. Babu alitoa agizo hilo , Aprili 26, 2025, alipotembelea, kukagua na kuweka jiwe la msingi katika shule hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kufuatia agizo hilo Babu amesikitishwa na ucheleweshaji wa ujenzi wa maabara licha ya serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni 500 kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza adha ya wanafunzi wa Kata ya Masama Rundugai waliokuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Bw. Michael Mumbuli, alieleza kuwa tayari yamekamilika majengo mawili ya madarasa yenye ofisi, jengo la utawala, maktaba, jengo la TEHAMA, matundu ya vyoo kwa wavulana na wasichana, kichomea taka, pamoja na ujenzi wa maabara ya kemia na baiolojia ambayo bado haijakamilika, sambamba na maabara ya fizikia.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masama Rundugai, Mhe. Waziri Simbano, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za miradi ya maendeleo inayosogeza huduma muhimu kwa wananchi wa eneo hilo.
Wakazi wa kata hiyo, akiwemo Bi. Jesca Peter, wameelezea kufarijika kwa mradi huo, wakikiri kuwa watoto wao walikumbwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta shule
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa