Serikali mkoani Kilimanjaro imewataka viongozi wa kisiasa na wananchi kutotanguliza maslahi binafsi ya kisiasa na vyama vya siasa na kushiriki ipasavyo katika mpango kabambe (Master Plan) wa Mji wa Moshi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa utayarishaji wa mpango huo uliowakutanisha madiwani na watendaji wa serikali katika ngazi mbalimbali,Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Sadiki M.Sadiki amesema ni vyema viongozi wakatathimini fursa mbalimbali za maendeleo zitakazowafikia wananchi wa mji wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro na kuachana kutanguliza maslahi binafsi ya wanasiasa na vyama vya sisiasa ambazo zitawachelewesha wananchi kufikia maendeleo.
Sadiki amesema kwa sasa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi iko kwenye maandalizi ya mpango mpya wa mwaka 2017-2037 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 142, kwa mujibu wa Gazeti la Serikali Namba 219 la Tarehe 15 Julai 2016.
Ameongeza kuwa mpango huo unahusisha kuongeza eneo la mji wa Moshi kwa kuongeza kilomita za mraba 68 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na kilomita za mraba 16 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Akifafanua zaidi Sadiki amesema kutokana na mpango huo kutakua na athari za mabadiliko katika wilaya ya Moshi na Hai kutokana na upanuzi wa mipaka kisheria na kuhusisha baadhi ya kata zilizopo katika wilaya hizo kuingia katika mji wa Moshi.
Sadiki ameongeza kuwa kufuatia upanuzi huo kutakuwa na mabadiliko ya kiutawala hivyo basi viongozi wa kisiasa wasiwe na hofu juu ya hatima zao kisiasa. “Kuna baadhi ya watu wafikiria juu ya hatima za udiwani wao endapo kata zao zitaingia ndani ya mji. ” alisema Mhe. Sadiki.
Aidha Mhe. Sadiki aliwataka wajumbe wote kuwapa ushirikiano wataalamu wa mipangomiji watakapowasilisha mpango huo na kutokuwa na hofu ya kukosa fursa za uongozi kwani kama kiongozi atahitajika na wananchi wataendelea kumchagua.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa