Mbio za Mwenge wa Uhuru zimehitimishwa Mkoani Kilimanjaro Aprili 8,2024 baada ya kukimbizwa katika halmashauri zote saba za Mkoa na kupitia miradi 47 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 29.34
Ikumbukwe kuwa mbio hizo zilizinduliwa rasmi Kitaifa Mkoani Kilimanjaro Aprili 2,2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) na kuanza kukimbizwa katika Manispaa ya Moshi na kuhitimishwa katika halmashauri ya Wilaya ya Same Aprili 8,2024.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amesema jumla ya miradi 47 yenye jumla ya thamani ya Shilingi Bilioni 29.34 imetembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri zote za Mkoa ambapo miradi hiyo 12 imewekewa Mawe ya Msingi, miradi 16 imezinduliwa na miradi 19 imetembelewa ikiwemo sekta ya Afya miradi 7, Barabara na madaraja miradi 6, Elimu miradi 7, Maji miradi 7, Utunzaji wa mazingira miradi 7, Vijana Miradi 7 na miradi mengineyo 6.
Mhe. Babu amesema hayo Wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Kilimanjaro kwenda Mkoa wa Tanga leo Aprili 9, 2024 katika viwanja vya Mazinde Mkoani Tanga.
Aidha, Mhe. Babu amesema Mwenge wa uhuru umepata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya makundi ya vijana wakiwemo wenye ulemavu na wanawake ambao wamedhamiria kuzalisha mali na kujiendeleza kiuchumi. Vilevile Mwenge wa uhuru umezindua klabu za kupambana na Rushwa, Madawa ya kulevya, Malaria, uhifadhi na uendelezaji wa mazingira.
Hata hivyo, Mhe. Babu amesema kuwa miradi yote iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 imechangiwa na Wananchi, Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa na dhamira ya kuendeleza falsafa ya kujitegemea.
Ameendelea kusema mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 zimejikita katika kukuza na kusimamia kwa karibu mabadiliko ya tabia nchi, hifadhi ya mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kukuza ushirikishwaji wa wadau wote kwa kuakisi kauli mbiu isemayo: - “Tunza mazingira, na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu’’.
Hivyo, Mkoa umeweza kuratibu zoezi la upandaji wa miti kutoka miti 7,857 mwaka 2022/2023 na hadi kufikia Februari, 2024 miti 8,709,200 imepandwa. Serikali na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamedhamiria kwa pamoja kurudisha uoto wa asili wa mkoa wa Kilimanjaro na mlima Kilimanjaro kwa kuzingatia Sera, sheria, kanuni na Taratibu za uhifadhi wa mazingira hivyo jumla ya miti 2,487,095 ikiwemo miti ya matunda imepandwa katika kipindi hiki cha mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 mkoani Kilimanjaro.
Mkoa umeendelea kuwahimiza wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki katika mapambano ya UKIMWI hivyo basi kiwango cha maambukizi ya VVU kwa Mkoa wa Kilimanjaro kimeendelea kushuka kutoka asilimia 3.9 mwaka 2011/12 hadi asilimia 2.6 mwaka 2016/17 kwa watu wa umri wa miaka 15 hadi 64. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa tafiti 4 za kitaifa zilizokwishafanyika hadi sasa.
Aidha, katika mikesha ya Mwenge wa Uhuru, jumla ya wananchi 2331 (Me 1443 na Ke 888) walijitokeza kupima maambukizi ya VVU na UKIMWI na waliokutwa na maambukizi ni wananchi 13 (Me 5 na Ke 8).
Hata hivyo Mhe. Nurdin Babu amewapongeza na kuwashukuru Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2024 wakiongozwa na Ndugu Godfrey Eliakimu Mnzava pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa waliyoifanya katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa