WAKINAMAMA Wajawazito katika kata ya Stesheni wilayani Same mkoani Kilimanjaro waliokuwa wakitembea umbali wa kilomita 10 kufuata huduma za afya hospitali ya wilaya wameondokana na adha hiyo baada ya Serikali kuikarabati zahanati ya Masandare.
Akizungumza Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi mara baada ya Mwenge kufika kuzindua zahanati hiyo alisema kuwa hapo awali ilikuwa inafanya kazi japo baadhi ya huduma zilikuwa hazitolewi katika zahanati hiyo.
Alisema kuwa, wananchi wa kitongoji cha Masandare walikuwa wakikabiliana na changamoto za miundombinu ya sekta ya Afya jambo ambalo lilikuwa likipelekea baadhi ya huduma kuzikosa katika eneo hilo lakini serikali iliona haja ya kwenda kuiboresha zahanati hiyo.
"Mwenge wa Uhuru umepata heshima kubwa ya kufika katika eneo hili ili kuonyesha matumaini, upendo kwa wananchi hivyo wananchi watakuwa na uhakika wa kupata huduma iliyo bora za Afya" Alisema Ussi.
Kiongozi huyo aliongeza "tunahitaji kupeana pongezi za hali ya juu kutokana na ukarabati wa zahanati hii ukiingia ndani unaona huduma ya mama na mtoto kwa hali ya ubora tunatambua wakinamama wetu hawa wanapokosa huduma ya kujifungulia katika eneo hili inakuwa ni changamoto kubwa".
Alisema kuwa, wakinamama hao Wajawazito walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 7-10 kufuata huduma katika hospita ya Same ambapo ni changamoto jambo ambalo linaweza likapelekea vifo vya kina mama na watoto.
Alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuitunza zahanati hiyo kwani Serikali imeshatimiza wajibu wake wa kuikarabati upya na kuweka mazingira safi na madaktari wataendelea kutoa huduma iliyo bora.
Awali akisoma taarifa za ukarabati wa zahanati hiyo, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Ally Said alisema kuwa ukarabati wake umegharimu milioni 50.
Alisema kuwa, toka kukamilika kwa zahanati hiyo jumla ya wamama 231 wamejifungua salama, watoto 711 wamepata chanjo, wajawazito 1050 wamehudhuria kliniki na wagonjwa wa nje 1750 wametibiwa.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa