RAIS SAMIA AZINDUA MRADI MKUBWA WA MAJI SAME - MWANGA - KOROGWE
Posted on: March 9th, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe na kueleza kuwa sasa wananchi wa maeneo hayo watanufaika na huduma ya maji masaa 24.
Katika uzinduzi huo, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha vijiji 10 vilivyo jirani na Bwawa la Nyumba ya Mungu vinaunganishwa haraka kwenye mtandao wa maji ili wananchi wake pia wawe sehemu ya wanufaika wa mradi huo.
Aidha, Rais ameitaka wizara hiyo kuwaharakishia wananchi huduma ya maji kwani mradi huo umefadhiliwa kwa mkopo, hivyo ni muhimu maji yaanze kutumika ili wananchi wachangie urejeshaji wa fedha hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Juma Aweso, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulikuwa na changamoto nyingi, ikiwemo hatua za kinidhamu dhidi ya watendaji waliochelewesha kazi, lakini hatimaye mradi umekamilika kwa mafanikio.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema mradi huo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Same, Mwanga na Korogwe, kwani utaboresha hali ya maisha na kuinua uchumi wa eneo hilo.Sambamba na hilo amempongeza Rais Samia kwa kutatua adha ya Maji kwa Wananchi wa maeneo hayo ambapo awali walitembea umbali mrefu kutafuta maji umbali mrefu.
Aidha, Mradi wa Maji wa Same - Mwanga - Korogwe unatajwa kuwa mradi mkubwa uliotekelezwa kwa muda mrefu ambapo zaidi ya bilioni 300 zimetumika kukamilisha mradi huo ambao kwa sasa utawasaidia Wananchi wa Maeneo hayo kupata maji kwa uhakika tofauti na awali.