Serikali Mkoani Kilimanjaro imewataka Watendaji pamoja na Madiwani kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ili kukuza uchumi wa Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai katika Baraza Maalumu la Madiwani la kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Wilayani Siha.
Mhe. Kagaigai alisema ushirikiano miongoni mwa Watendaji na Madiwani utasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Mkurugenzi ninakupongeze licha ya kuwa umekaa hapa kwa muda mfupi lakini umezichambua hoja kwa umakini na kwa kiwango kikubwa, madiwani endelezeni ushirikiano na simamieni mapato na matumizi, wakati huo huo mbuni vyanzo vipya vya mapato, " alisema Mkuu wa Mkoa
Aidha Mhe. Kagaigai alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Bw. Ndaki Mhuli, kuhakikisha anaongeza umakini kwa kuboresha Kitengo cha Ukaguzi wa ndani ili kimsaidie kujitathimini kwa kina wakati changamoto zinapotokea.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro. Dkt. Seif Shekalaghe amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa maandalizi mazuri ya kikao ikiwa ni pamoja na taarifa kuwa na hoja ambazo hazijafungwa na kutoa sababu za kutojibiwa kwa hoja hizo hadi sasa, jambo ambalo limerahisisha mjadala kwenye kikao.
Awali akisoma taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Bw. Mhuli alisema tayari amekijulisha kikao kuwa Halmashauri imeshatatua changamoto zilizokuwepo hususani kwenye
kuongeza mapato pamoja na kufunga hoja zilizoainishwa na CAG.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa