Halmashauri ya Wilaya ya Hai imetakiwa kutekeleza ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri juu ya hoja za Mkaguzi ambazo hazijafungwa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai katika Baraza Maalumu la Madiwani la kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Wilayani Hai.
Aidha amemuelekeza Katibu Tawala Mkoa kufuatilia baadhi ya hoja ambazo zinajirudia katika kila halmashauri. Akitoa mfano wa hoja ya dawa ambazo zimeisha muda wake wa matumizi Mhe. Kagaigai amesema hoja hii inapaswa kufungwa kwa kufuata taratibu zilizopo na kuziteketeza.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato Mhe. Kagaigai amesema Halmashauri zingine ziko hatua nzuri za ukusanyaji wa mapato ukilinganisha na Halmashauri ya Hai iliyokusanya asilimia 74% ya mapato, amesema hii inatokana na kutokufanya ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato kwa baadhi ya maeneo. Hata hivyo amewaelekeza Watendaji wa Halmashauri hiyo kufuatilia vyanzo vya ukusanyaji wa mapato hayo napia kujitahidi kubuni vyanzo vipya ambavyo vinaweza kuwaingizia mapato.
Katibu Tawala Mkoa Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na kupokea maelekezo ya Mhe. Mkuu wa mkoa ametoa ushauri kwa Halmashauri hiyo kwa kuwapa njia ambazo zitasaidia kutojirudia kwa hoja. Amesema kila mtu akiwajibika kwa nafasi yake itasaidia kupunguza tatizo hilo, kufanya kazi kama timu, kuchukua hatua kwa wakati, kubadilika kwa kuwa wazalendo na kufuata taratibu zinazohusika.
Mweka hazina wa Halmashauri hiyo Juma Kasoga akiwasilisha taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ameshauri Baraza la halmashauri hiyo kufuata sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2013 ili kutojitokeza kwa mapungufu madogomadogo wakati wa ukaguzi.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa