Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utawala Bora ili waweze kufanya kazi zao bila kukiuka maadili ya uongozi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai baada ya kuwaapisha Wakuu Wapya wa Wilaya walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuongoza Wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro.
Aidha, Mhe. Kagaigai amewakumbusha Wakuu hao wa Wilaya kulipa kipaombele suala zima la usalama wa wananchi na mali zao kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na Usalama.
Mbali na hayo Mhe. Mkuu wa Mkoa amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanazielewa kero za wananchi na kuzitatua kwa weledi, uadilifu na bila ubaguzi wala upendeleo wowote.
Awali akitoa nasaha zake kwa Wakuu wa Wilaya Shekh Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shekh Shabani Mlewa amewaasa viongozi hao kuwa mfano wa kuigwa na jamii kwa tabia na mienendo mema ili malengo ya wananchi katika maeneo yao yaweze kutimia.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya ambaye ni miongoni mwa wakuu wa wilaya walioapishwa amewaahidi wananchi na Mhe. Mkuu wa Mkoa kutoa ushirikiano kwa wananchi na wadau wote wa maendeleo katika wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro kwa Ujumla.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa