Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa, kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, kufanya tathmini na kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Mabogini - Kahe yenye urefu wa kilomita 31.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuendelea kutatua changamoto za wananchi, hususan katika sekta za miundombinu na huduma muhimu za kijamii kama vile shule na vituo vya afya, kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na huduma bora.
"Barabara hii muhimu kwa wananchi wa Mabogini na Kahe lazima ianze kujengwa mara moja kabla ya mwaka mpya wa bajeti. Tumeipanga kuingiza katika mpango wa TACTIC kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia (World Bank) na itajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 45," alisema Waziri Mchengerwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, amewataka wananchi wa maeneo husika kuendelea kuwa wavumilivu na kuiamini Serikali wakati utekelezaji wa mradi huo ukisubiriwa kuanza rasmi.
Wananchi wa Kata ya Mabogini na Kahe wameonesha shukrani zao kwa ujio wa Waziri Mchengerwa na kueleza imani yao kuwa changamoto waliyoishi nayo kwa miaka mingi sasa imepata mwarobaini.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa