TAARIFA KWA UMMA
ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2022 KATIKA
MKOA WA KILIMANJARO
Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi yanavyoendelea. Aidha, ninapenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mkutano huu.
Jambo lililonifanya niwaite leo hii, ni kuwapeni taarifa kwa hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi kwa Mkoa wa Kilimanjaro.
Ndugu Waandishi wa Habari, maandalizi ya Sensa yamekamilika kwa asilimia 96. Hatua ya pili ni kuanza kwa zoezi lenyewe ambalo limeanza jana tarehe 21/08/2022 kwa kukusanya taarifa za huduma za jamii zilizopo katika maeneo yote ya Mkoa wetu. Zoezi hili linatarajia kukamilika leo tarehe 22/08/2022.
Usiku wa kuamkia tarehe 23/08/2022. Ni siku ya Sensa na itabaki kuwa tarehe rejea ya siku ya Sensa. Zoezi la Sensa litaendelea kwa takribani siku 6 hadi 7 kwa kuzingatia tarehe rejea. Aidha baada ya siku ya saba itafuatia Sensa ya Majengo itakayofanyika kwa muda wa siku tatu. Ieleweke kuwa Sensa haiwezi kukamilika kwa siku moja.
Pamoja kwamba ni siku ya mapumziko, inawezekana baadhi ya kaya zisifikiwe kutokana na wingi wa kaya, hivyo unachotakiwa kufanya ni kuorodhesha na kuandika kwenye karatasi taarifa ya watu wote watakaolala kwenye kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa ya tarehe 23 Agosti 2022 ili karani atakapofika kwenye kaya hiyo; Mkuu wa kaya au mwanakaya atakayekuwepo aweze kutoa taarifa hizo. Hii ni muhimu kwa kaya na kwa karani wa Sensa kurahisisha zoezi hili muhimu. HAPA NAWEKA MSISITIZO, NAOMBA WANA KAYA TUZINGATIE HILI KWA UFANISI WA ZOEZI LETU HILI MUHIMU.
Taarifa muhimu za kila mwanakaya za kuziandaa ni pamoja na: -
1. Jina kamili (3)
2. Jinsi
3. Umri
4. Hali ya ndoa
5. Namba ya simu
6. Namba/kitambulisho cha NIDA, kadi ya mpiga kura, leseni au cheti cha kuzaliwa.
7. Taarifa za Elimu
8. Taarifa za hali ya ulemavu
9. Umiliki wa Ardhi, Majengo, vifaa/rasilimali
10. Taarifa ya Shughuli za Kiuchumi
11. Namba ya mita ya Umeme (Tanesco) pamoja na taarifa nyingine muhimu.
Mkoa umejipanga kuhakikisha kila mtu na kila kaya inapitiwa na kuhesabiwa.
Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kutoa wito kwa wamiliki wote wa nyumba za kulala wageni (Hotel, Lodge, Guest) na kambi za watalii kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha kuwa wateja wote watakaolala katika nyumba hizo usiku wa tarehe 22 Agosti kuamkia tarehe 23 Agosti 2022 wanajaza fomu maalum ambayo imepelekwa kwa kila nyumba ya wageni. Aidha, makundi mengine kama wasafiri, watu wasio na makazi maalum hususani watoto/vijana wa mitaani watahesabiwa kwa Utaratibu maalum usiku wa kuamkia tarehe 23 Agosti 2022.
Matokeo ya takwimu za Sensa ya mwaka 2022 yataiwezesha Serikali kupima kiwango cha maendeleo kilichofikiwa na kupanga mipango ya maendeleo kwa wakati ujao. Takwimu zinazotokana na Sensa huwezesha utoaji huduma za Maji, Elimu, Afya kwa kuzingatia idadi ya watu. Jambo la kipekee katika Sensa hii ni kuwa tutapata takwimu za Idadi ya watu katika ngazi ya Kitongoji/Mtaa.
Sensa huwezesha Serikali kupanga makadirio ya matumizi yanayokidhi matakwa ya Wananchi na maeneo wanayoishi, kwa kuzingatia umri, jinsia, elimu, ajira zao na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Nichukue fursa hii pia kuwataka watendaji wote wa kata, vijiji, wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa yote ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro kutoa hamasa kwa wananchi wa maeneo yao na ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa Sensa watakapokuwa katika maeneo yenu ya kiutawala.
Ninawaelekeza Wakuu wote wa Wilaya kufuatilia mwenendo wa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi katika wilaya zao ikiwa ni pamoja na Usalama wa makarani na vitendea kazi vyao.
Ndugu Waandishi wa Habari, naomba niendelee kuwapongeza sana na kuwashukuru kwa ushirikiano mnaoutoa kila siku, napenda kutumia fursa hii kuwasisitiza muendelee kutangaza taarifa hizi kwa usahihi na kwa wingi ili kuusaidia mkoa wetu kupata takwimu sahihi za Idadi ya Watu na Makazi yao.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Nurdin H. Babu
MKUU WA MKOA
22 Agosti 2022
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa