Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu leo Februari 1,2023 ameapisha Wakuu wa Wilaya watatu (3) akiwepo Mkuu wa wilaya ya Siha Mhe. Dkt. Christopher D. Timbuka, Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Kasilda J. Mgeni na Mkuu wa wilaya ya Hai Mhe. Amir M. Mkalipa.
Wakati wa hafla hiyo ya uapisho Mhe. Babu amewasisitiza Wakuu hao wa Wilaya kusimamia misingi ya haki, utawala wa sheria na maadili katika kutekeleza majukumu yao kwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwa weledi, uadilifu na bila ubaguzi wala upendeleo wowote katika maeneo yao, vilevile kuwa karibu na wawe wanafikika kirahisi kwa wanaowaongoza ili wananchi, viongozi na wadau mbalimbali waweze kuwasilisha mawazo yao na changamoto zao na kuzifanyia kazi ama kuzitatua kwa wakati.
Aidha, amewaelekeza kusimamia amani na usalama wa wananchi na mali zao, vilevile watambue wao ndio Wenyeviti wa kamati za Usalama katika ngazi za wilaya wakisaidiwa na vyombo vya Usalama hivyo wakashirikiane na vyombo vya Usalama, kupitia kamati ya usalama katika kufanya maamuzi makubwa ya Wilaya.
Hata hivyo, Mhe. Babu amewasisitiza Wakuu wa Wilaya kusimamia suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na Kuhakikisha mapato hayo yanatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi pia waendelee kusimamia udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali na kuzuia ubadhilifu, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote wataokiuka taratibu jambo hilo lifanyike kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo pamoja na Kanuni.
Kwa upande wa zoezi la Uandikishaji kwa wanafunzi wa Awali, Darasa la Kwanza pamoja na wanaojiunga na Kidato cha kwanza kwa mwaka 2023. Mhe. Babu amewataka kufuatilia na kujiridhisha na utoaji sahihi wa makisio au maoteo ya takwimu mbalimbali kutoka katika halmashauri zao pia uandikishaji wa wanafunzi bila kusahau utoaji wa takwimu sahihi, utatoa fursa na nafasi ya Wilaya na Mkoa kujipanga vizuri katika utekelezaji wa mipango katika majukumu yetu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mhe. Patrick Boisafi katika hafla hiyo amewaambia Wakuu wa Wilaya waliobaki katika wilaya zao na Wakuu wa Wilaya wapya kuwa wao ni kitu kimoja hakuna haja ya kukinzana, ameendelea kusema wametumwa kufanya kazi na kutumikia wananchi hivyo watoe ushikiano kwa Wakurugenzi pamoja na viongozi wengine wa wilaya.
Ameendelea kusema wananchi wanataka kuona maendeleo, maji ,umeme, barabara, miundombinu, elimu na kuona watu wako salama, wakifanya hivyo watawaandalia uchaguzi ulio wa haki na salama.
Vile vile amewasisitizia wakuu hao kuendelezea yale yote yaliyoachwa na wenzao kwani maendeleo ni yetu sote pia kusimamia vyema miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita vile vile kutekeleza ilani ya Chama Cha
Mapinduzi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe. Amir M. Mkalipa kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya walioapishwa amesema wapo tayari kufanya kazi kwa nguvu zote, maarifa na juhudi zao na kupokea maelekezo yote yatakayotoka kwenye ngazi zinazowahusu.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa