Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), amezindua rasmi mbio za Mwenge wa Uhuru leo Aprili 2,2024 katika uwanja wa chuo kikuu cha Ushirikia Moshi.
Wakati wa hafla ya uzinduzi wa mbio hizo amewataka wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kulitendea haki taifa kwa kufanya kazi waliyoaminiwa na kuhakikisha wananchi wanaondoka na ujumbe uliokusudiwa wa kuhamasisha tunu za taifa ambazo ni amani, uzalendo, umoja na mshikamano ndani ya Taifa na pia kuchochea shughuli za maendeleo.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 umebeba ujumbe wa uchaguzi na utunzaji mazingira hivyo amewasisitiza wananchi kwamba uchaguzi ni haki ya kila mtanzania kuchagua na kuchaguliwa na hivyo anawakumbusha kuhakiki jina katika daftari kabla ya zoezi la upigaji kura pamoja na kutunza mazingira katika maeneo yote kwa kupanda miti kwenye makazi yao na kutunza vyanzo vya maji.
Vilevile Mhe. Majaliwa amesisitiza wananchi juu ya kuzingatia lishe bora, kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI,kujikinga na ugonjwa wa malaria, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na dawa za kulevya..
Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Mwita amesema baada ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwa siku 195 katika mikoa 31 na halmashauri 195. Amesema vijana 6 ambao ni wakimbiza Mwenge kitaifa wataenda kuwakumbusha wananchi juu ya historia na uzalendo wa nchi yao.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Mwenge wa Uhuru wa Mwaka huu ni maalumu hii ni kutokana na kubeba 60 tatu ambazo 60 ya kwanza ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, 60 ya pili Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na 60 ya tatu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema Mwenge wa Uhuru huleta huduma kwa wananchi karibu za kiuchumi na kijamii, kuimarisha uzalendo, kuondoa ukabila na kuunganisha taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amesema jumla ya miradi 47 yenye thamani ya Tshs. Bilioni 29,340,412,701.88 itatembelewa, kuwekewa mawe ya msingi na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru, kati ya miradi hiyo 12 ni yakuwekewa mawe ya msingi, 16 yakuzinduliwa na 19 ni ya kutembelewa.
Aidha, Mhe. Babu amesema katika kipindi cha miaka 3 ya Uongozi wa awamu ya Sita mkoa wa umepokea jumla ya Tshs. Bilioni 828.75 fedha ambazo zimetekeleza miradi 1,190 ya maendeleo katika sekta ya afya,elimu, miundombinu ya barabara, maji, kilimo, mifugo, usafirishaji na uchukuzi, mipingo miji, utalii na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa