Zaidi ya wananchi 324,797 katika vijiji 179 mkoani Kilimanjaro wanaenda kunufaika na huduma ya maji safi baada ya serikali kutenga kiasi cha Tshs. Bilioni 12.3 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika utekelezwaji wa miradi ya maji 27.
Aidha, Serikali imetoa kiasi cha Tshs. Bilioni 3.5 kutoka kwenye fedha za mpango wa ustawi wa Taifa na mpambano dhidi ya UVIKO-19 zitakazotumika kutekeleza miradi ya maji 7 katika wilaya zote sita za mkoa wa Kilimanjaro.
Ameyasema hayo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai wakati wa uzinduzi wa wiki ya maji Machi 16,2022 mkoani hapa na kuwaelekeza RUWASA kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kutosita kuwachukulia hatua wanaoshindwa kufanya kazi kwa utaratibu uliowekwa.
Mhe. Kagaigai amesema Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) imetengewa kiasi cha Tshs. Bilioni 16 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwa mwaka wa fedha 2021/22. Amesema mamlaka hiyo imefanya usanifu wa kuboresha huduma ya maji katika maeneo mapya ya huduma ya Kata 12 katika halmashauri ya Moshi na thamani ya utekelezaji wa miradi hiyo ni Tshs. Bilioni 11.3 na kufikia hadi sasa mamlaka imetekeleza miradi hiyo kwa asilimia 31.68 kwa thamani ya Tshs. Bilioni 2.7.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa bonde la maji mto pangani Segule Segule amesema pamoja na kutunza vyanzo vya maji wameendelea kuweka mipaka ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
Mkuu wa kitengo cha mipango na biashara wa MUWSA, Tumaini Marandu amesema Mamlaka imepanga kutekeleza miradi minne kwa kuongeza kiwango cha maji kufikia mita za ujazo 23,067. Amesema vyanzo vinavyoongezwa ni chemchemu ya Karanga mita za ujzo 2,592, Miwaleni mita za ujazo 2,592, Mkolowonyi mita za ujazo 1,296 na Njoro ya Dhobi mita za ujazo 16,587.
Florida Street
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: 027 2758248/027 2751
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz/ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa