Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, amewasihi Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutumia vyema fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kufikia malengo yao ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Babu ametoa wito huo leo, Mei 14, 2025, wakati wa semina ya kuwawezesha vijana na wanawake kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya CRDB kupitia programu ya CRDB Foundation.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ndani ya nchi katika kuhakikisha maisha ya wananchi, hususan wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, yanaboreshwa kupitia mikopo hiyo. Hata hivyo, ameonya kuwa mikopo hiyo haitaleta tija endapo itachukuliwa bila mipango madhubuti.
Aidha, ameitaka Benki ya CRDB kuendelea kutoa elimu na semina kama hiyo katika wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro, zikiwemo Mwanga, Same, Rombo, Siha, na Hai, ili kuhakikisha walengwa wote wanapata uelewa wa namna bora ya kutumia mikopo hiyo kwa maendeleo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mikopo kutoka Benki ya CRDB, Bw. Xavery Makwi, amesema kuwa hadi kufikia mwisho wa mwezi Machi mwaka huu, benki hiyo imefanikiwa kutoa mafunzo kwa zaidi ya wananchi milioni moja – wakiwemo vijana na wanawake – na mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 za Kitanzania.
Elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030, ambayo inalenga kujenga uchumi imara unaotegemea rasilimali watu wenye ujuzi na maarifa.
17 Barabara ya Florida
Anuani ya Posta: P. O. Box 3070, Moshi
Simu: +255 (027) 2754236/7
Mobile:
Anuani pepe: ras@kilimanjaro.go.tz / ras.kilimanjaro@tamisemi.go.tz
Hakiimiliki©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.Haki zote zimehifadhiwa